2.1 Hali ya malezi kwa watoto na vijana.
Hivi sasa nchi nyingi ulimwenguni ikiwemo Tanzania kuna mporomoko mkubwa wa maadili. Wazazi ndani ya jamii wanalalamika juu ya watoto wa kizazi hiki kuwa wamekosa maadili.
Lakini wazazi hawa wanasahau kuwa kuporomoka kwa maadili ya watoto wao kunatokana na wao kutokuwalea katika misingi mizuri ambayo ni Neno la Mungu. Huko Ulaya na Marekani wazazi/mataifa walibweteka na maendeleo ya kiuchumi, teknolojia, sayansi na maisha bora kimwili na kusahau tunu kubwa inayotokana na maendeleo ya kiroho(spirituality). Makuzi ya kiroho hujenga maadili na hivyo kujenga utu wa mtu.
Katika nchi hizi watu wengi hasa kundi la vijana sasa hivi hawaendi Kanisani au Misikitini Kuabudu. Wamejitenga kabisa na Mungu na katika baadhi ya nchi Makanisa yameuzwa na kutumika kwa shughuli nyingine kabisa kama vile maduka na hata pia kugeuzwa kuwa sehemu za burudani kama vile sehemu za kuuzia vileo na starehe zingine.
Aidha katika nchi hizi tunashuhudia ongezeko kubwa la mporomoko wa maadili ya asili ya mwanadamu. Katika nchi hizi sasa tunashuhudia uhalalishwaji kisheria wa ndoa na mapenzi ya watu wa jinsia moja, ongezeko la vitendo vingine viovu ambavyo ni chukizo mbele za Mungu.
Nchi za kiafrika nazo hazijasalimika na hali hiyo. Mporomoko mkubwa wa maadili katika nchi za Afika unazidi kuongezeka na kushamiri kutokana na utandawazi. Nchi zetu sasa zinashuhudia ongezeko kubwa la vitendo viovu kila siku,vingi vikifanywa na kundi la vijana. Wazazi walio wengi wameacha wajibu wao wa asili wa kuwalea watoto wao na kuwarithisha maadili ambayo huleta ustawi wa mtu mmoja mmoja na jamii/taifa.
Wazazi wengi hawaendi na watoto wao Makanisani na Misikitini wala hawaoni umuhimu wa watoto wao kupata mafundisho ya dini tangu wakiwa watoto ili wakue na kustawi katika msingi wa Neno la Mungu. Maovu mengi tunayoyashuhudia katika jamii ni kutokana na watu kukosa msingi wa Neno la Mungu ambalo likikaa katika myoyo huwafanya watu kuwa na hofu ya Mungu na hofu hiyo huwafanya wajiepusha na matendo maovu kwa kujua kwamba hayampendezi Mungu na yana hukumu.
Hivi sasa tunashuhudia hofu ya Mungu ikizidi kupungua katika nchi yetu, na hivyo kutishia amani na utangamano katika taifa letu. Vitendo viovu vinaongezeka kwa kasi katika taifa letu kwa sababu watu wamekosa hofu ya Mungu.
Rais wetu mpendwa wa awamu ya Tano Marehemu Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli amekuwa akituasa mara nyingi kwamba tumwogope Mungu, maana yake tufanye yale yanayompendeza Mungu na tuache matendo maovu. Matendo mema huleta afya kwa jamii/taifa lolote.