MPANGO WA KUWAPATIA MAANDIKO MATAKATIFU (BIBLIA) WATOTO, VIJANA NA WAFUNGWA MAGEREZANI NCHINI TANZANIA.
1. UTANGULIZI.
Chama cha Biblia cha Tanzania (CBT) ni shirika la Kikristo lililoandikishwa mwaka 1970 na kupewa nambari S0 5722. Ni mwanachama wa Muungano waVyama vya Biblia Ulimwenguni(United Bible Societies (UBS). Shirika hili ni chombo cha Kanisa la Tanzania ambalo kazi yake kubwa na ya msingi ni kuwapelekea watu wote hapa nchini Tanzania Habari njema ya Yesu Kristo kwa kutafsiri, kuchapisha na kusambaza Biblia ikiwa katika lugha anayoielewa msomaji, bei anayoiweza na mfumo anaoupendelea.
Tangu kusajiliwa kwake hapo mwaka 1970, Chama cha Biblia cha Tanzania kimekuwa kikitekeleza majukumu yake hayo kwa ushirikiano mkubwa na wa karibu na makanisa yote ya Kiprotestanti, Katoliki, Sabato na Kipentekoste hapa Tanzania; na pia kwa ushirikiano mkubwa na wa karibu na Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni (United Bible Societies-UBS) ambalo ni ushirika wa vyama vyote vya Biblia katika nchi zote.
Chama kimeweza kufanya tafsiri na kinaendelea kutafsiri Biblia katika lugha mbalimbali za makabila ya hapa Tanzania. Kutafsiri Biblia katika lugha mbalmbali za makabila kunafanyika kwa malengo makuu mawili. Lengo la kwanza la kufanya tafsiri hizi ni kwa kuamani kuwa watu wanaweza kulielewa Neno la Mungu kwa urahisi zaidi wakisoma au kuelezwa katika lugha zao na kuainisha na mazingira halisi ya mazingira yao.
Lengo la pili ni kusaidia kutunza lugha za makabila kwa faida ya vizazi vijavyo vya kabila husika, kwani mila na utamaduni wa kabila zipo katika lugha ya watu wa kabila husika. Tangu kuanzishwa kwake Chama cha Biblia kimefanya tafsiri kadha na kuzisambaza hapa nchini zikiwamo Biblia katika lugha za:
- Kiswahili
- Kimaasai,
- Cigogo
- Iraqw
5. Nyakyusa
6. Igikuria
7. Ruhaya
8. Kisukuma
9. Kidatooga
10. Kimashami
11. Kivunjo
12. Kimochi
Baadhi ya Biblia ambazo kwa sasa zipo katika hatua mbalimbali za tafsiri ni:
- Kihehe
- Cikaguru
- Kinyamwezi
- Chasu(Kipare)
5. Kifipa
6. Kinyiha
7. Kinyiramba
8. Kirimi( Kinyaturu)
9. Kiha
Agano Jipya.
- Kimeru
- Kibena
- Kishambala
- Kikinga
5. Kijita
6. Kifipa
7. Kizaramo
2.0 Umuhimu wa Neno la Mungu kwa maendeleo
Tunapoangalia historia ya ustawi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ulimwenguni kote, tunaona kuwa jamii ambazo zilijengwa katika misingi ya Neno la Mungu zilistawi kimaendeleo ikilinganishwa na zile ambazo ama hazikuamini au zilimuasi Mungu. Neno la Mungu likiwa ndani ya myoyo ya watu huzaa upendo ambao huzifanya jamii kuwa zenye amani na utangamano, tunu ambazo husaidia kuweka mazingira wezeshi kwa watu kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
2.1 Hali ya malezi kwa watoto na vijana.
Hivi sasa nchi nyingi ulimwenguni ikiwemo Tanzania kuna mporomoko mkubwa wa maadili. Wazazi ndani ya jamii wanalalamika juu ya watoto wa kizazi hiki kuwa wamekosa maadili.
Lakini wazazi hawa wanasahau kuwa kuporomoka kwa maadili ya watoto wao kunatokana na wao kutokuwalea katika misingi mizuri ambayo ni Neno la Mungu. Huko Ulaya na Marekani wazazi/mataifa walibweteka na maendeleo ya kiuchumi, teknolojia, sayansi na maisha bora kimwili na kusahau tunu kubwa inayotokana na maendeleo ya kiroho(spirituality). Makuzi ya kiroho hujenga maadili na hivyo kujenga utu wa mtu.
Katika nchi hizi watu wengi hasa kundi la vijana sasa hivi hawaendi Kanisani au Misikitini Kuabudu. Wamejitenga kabisa na Mungu na katika baadhi ya nchi Makanisa yameuzwa na kutumika kwa shughuli nyingine kabisa kama vile maduka na hata pia kugeuzwa kuwa sehemu za burudani kama vile sehemu za kuuzia vileo na starehe zingine.
Aidha katika nchi hizi tunashuhudia ongezeko kubwa la mporomoko wa maadili ya asili ya mwanadamu. Katika nchi hizi sasa tunashuhudia uhalalishwaji kisheria wa ndoa na mapenzi ya watu wa jinsia moja, ongezeko la vitendo vingine viovu ambavyo ni chukizo mbele za Mungu.
Nchi za kiafrika nazo hazijasalimika na hali hiyo. Mporomoko mkubwa wa maadili katika nchi za Afika unazidi kuongezeka na kushamiri kutokana na utandawazi. Nchi zetu sasa zinashuhudia ongezeko kubwa la vitendo viovu kila siku,vingi vikifanywa na kundi la vijana. Wazazi walio wengi wameacha wajibu wao wa asili wa kuwalea watoto wao na kuwarithisha maadili ambayo huleta ustawi wa mtu mmoja mmoja na jamii/taifa.
Wazazi wengi hawaendi na watoto wao Makanisani na Misikitini wala hawaoni umuhimu wa watoto wao kupata mafundisho ya dini tangu wakiwa watoto ili wakue na kustawi katika msingi wa Neno la Mungu. Maovu mengi tunayoyashuhudia katika jamii ni kutokana na watu kukosa msingi wa Neno la Mungu ambalo likikaa katika myoyo huwafanya watu kuwa na hofu ya Mungu na hofu hiyo huwafanya wajiepusha na matendo maovu kwa kujua kwamba hayampendezi Mungu na yana hukumu.
Hivi sasa tunashuhudia hofu ya Mungu ikizidi kupungua katika nchi yetu, na hivyo kutishia amani na utangamano katika taifa letu. Vitendo viovu vinaongezeka kwa kasi katika taifa letu kwa sababu watu wamekosa hofu ya Mungu.
Rais wetu mpendwa wa awamu ya Tano Marehemu Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli amekuwa akituasa mara nyingi kwamba tumwogope Mungu, maana yake tufanye yale yanayompendeza Mungu na tuache matendo maovu. Matendo mema huleta afya kwa jamii/taifa lolote.
2.2 Kwa nini Biblia kwa Watoto, Vijana na Wafungwa?
Katika nchi nyingi duniani na hasa nchi zinazoendelea watoto umri kati ya miaka 1-14 huwa ni rika yenye watu wengi zaidi, wakifuatiwa kwa wingi na kundi la vijana(miaka 15-24).
Makundi haya mawili haya kwa pamoja hapa Tanzania idadi yake ni zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu wote. Kutokana na wingi na umri, makundi haya yanayohitaji kuangaliwa /kutazamwa kwa karibu sana kwa maana ya malezi kwa maana ya kupewa huduma muhimu zitakazowafanya wakue na kustawi kiroho na kuwa raia wema wenye kupenda amani na ustawi wa taifa.
Wafungwa ni kundi la watu ambao wako gerezani kwa sababu ya kutenda makosa katika jamii na kukosesha wengine amani na utangamano. Kwahiyo, hili nalo ni kundi muhimu la kutazamwa katika malezi hasa ya kiroho ili wahusika (wafungwa) wanapomaliza kutumikia vifungo vyao waweze kuacha tabia mbaya za uhalifu na kuwa raia wema.
2.3 Mapendekezo ya na ushauri wa Chama cha Biblia kwa serikali katika kukabiliana na mporomoko wa maadili kwa wototo na vijana.
Chama cha Biblia cha Tanzania kinaishukuru sana Serikali yetu kwa kuruhusu Neno la Mungu kufundishwa mashuleni, jambo ambalo nchi zingine haziruhusu. Tunaamini hatua hii ni kwa kutambua kwamba mashuleni ndiko wanapoandaliwa viongozi wa taifa la kesho, kwa hiyo kuona umuhimu wa kuwapa malezi ya kiroho.
Tunakumbuka miaka ya nyuma serikali iliruhusu uanzishwaji wa chama cha “ Elimu ya Dini Mashuleni Tanzania”(EDIMASHUTA) ikiwa ni njia mojawapo ya kutoa fursa kwa watoto ya kupata mafundisho ya dini ili waweze kukua kimaadili kupitia dini zao. Hii ilikuwa ni fursa muhimu sana kwa wototo kujifunza somo la dini na hivyo kukua na kustawi katika misingi ya kuwa na hofu ya Mungu.
Chama cha Biblia cha Tanzania kilikuwa mshirika mkubwa katika mpango wa Elimu mashuleni kwa kutoa Biblia zilizotumiwa kama kitabu cha kiada mashuleni katika mafundisho hayo. Katika mpango huu, serikali ililifanya somo la dini kuwa la kutahiniwa na ilikuwa na “alama” (credit).
Kutokana na utambuzi huo vijana mashuleni walikuwa na bidii ya kujifunza somo la dini. Kwa njia hiyo waliweza kujengwa vizuri kiimani, kimaadili na kiustawi kwa ujumla na kundi hilo lilizaa viongozi waadilifu wa nchi yetu, kanisa na sekta binafsi.
Hata hivyo baadaye utaratibu wa somo la dini kuwa la kutahiniwa na lenye hadhi ya credit sawa na masomo mengine uliondolewa na hivyo kuwavunja moyo watoto na vijana katika kujifunza somo la dini.
Tunapendekeza kwamba somo la dini liendelee kufundishwa na lipewe hadhi/lihesabiwe sawa na masomo mengine katika mitihani, ili liweze kuchochea ari kwa watoto na vijana kujifunza somo la dini na hivyo kujengwa kimaadili.
2.4 Kwa nini Biblia sasa kwa vijana mashuleni.
Kwa kuangalia mwenendo wa maadili kwa vijana wetu mashuleni,na kuna umuhimu wa kurejesha somo hilo kwani umuhimu wake umeanza kuonekana. Kumekuwa na mmomonyoko wa maadili kwa vijana wetu sasa, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walilelewa katika misingi ya neno la Mungu.
Sasa hivi tunashuhudia vitendo viovu vikiongezeka katika jamii, ambapo watoto na vijana wanahusika. Jambo la pili tunaona mifano ya wenzetu nchi za Ulaya ambako utandawazi umewafanya wasitambue utu wa mtu.
Baadhi ya shule ambazo zimeendelea kufundisha somo la dini ni ushuhuda tosha kuonyesha namna somo la dini lilivyo muhimu katika ustawi wa mwanadamu. Shule hizi zimekuwa mfano mzuri kwa maadili na ufaulu mzuri wa masomo hata yasiyo ya dini.
Chama cha Biblia kinaona kwamba kuna umuhimu wa kurudisha somo la dini kwa shule zote za serikali na za binafsi na kulifanya somo la dini kuwa na hadhi ya kutahiniwa sawa na masomo mengine.
3.0 Mpango wa Chama cha Biblia cha Tanzania wa kuwapatia Biblia Watoto na Vijana mashuleni na Wafungwa magerezani.
Kwa kutambua umuhimu huo, Chama cha Biblia cha Tanzania katika mpango mkakati wa miaka mitano (2018 – 2022) kilianzisha mpango maalum wa kuhamasisha Makanisa na watu wenye mapenzi mema kushiriki kwa kuchangia fedha kwa ajili ya upatikanaji wa Biblia ili zisambazwe kwa wingi kwa watoto, vijana na wafungwa ikiwa ni moja ya vipau mbele vyake katika kipindi hiki cha miaka mitano.
Mpango huu unalenga makundi matatu ya watoto na vijana kwa rika na wafungwa walioko magerezani.
Na. |
Watoto |
Vijana |
Wafungwa magerezani |
1. |
Miaka 3 – 5 |
Miaka 16 – 24 |
Wanaume |
2. |
Miaka 6 – 9 |
|
Wanawake |
3. |
Miaka 10 -15 |
|
|
Katika mkakati wa kutekeleza mpango huu Chama cha Biblia cha Tanzania kilianza kwa kuwashirikisha viongozi wa makanisa kutokana na nafasi yao ya asili ya kuwajenga na kuwalea watu kiroho.
Pili kimewashirikisha wadau wengine wenye mapenzi mema wanaotamani kuona Tanzania inajengwa katika misingi imara ya kiroho na hivyo kuwa na taifa lenye watu wenye hofu ya Mungu.
Mpango huu umepata uungwaji mkono mkubwa sana na Kanisa la Tanzania, hali ambayo imetutia moyo sana Chama cha Biblia cha Tanzania, kwani tunatambua kwamba Kanisani ndiko Neno la Mungu linafundishwa na ndiko Wakristo wanaofanya Kanisa la Tanzania waliko.
Tunaamini mpango huu unatekelezeka na walengwa na taifa zima litanufaika.
3.1 Watoto na Vijana walengwa.
Mpango huu katika awamu hii ya kwanza unalenga watoto na vijana walioko katika shule kwa sababu ya urahisi wa kujua idadi yao na urahisi wa kuwafikia.
Hata hivyo shule zitazopewa kipaumbele ni zile zilizoko vijijini, ambazo mbali kuwa nyingi, lakini ndizo zenye watoto na vijana wengi wenye wazazi wenye hali duni ya uchumi; na hivyo hawana uwezo wa kuwapata/kuwanunulia watoto mahitaji yao kwa utoshelevu.
Ni kutokana na ukweli huo Chama cha Biblia cha Tanzania kinalenga kuwapatia watoto na vijana Biblia kwa bei nafuu ambayo wazazi wengi pamoja na hali yao duni kiuchumi wanaweza kuimudu.
3:2 Ufundishaji wa somo la dini mashuleni.
Kama tulivyoeleza katika utangulizi, Chama cha Biblia kinaona kwamba kuna umuhimu wa kurudisha somo la dini kwa shule zote za serikali na za binafsi na kulifanya somo la dini kuwa na hadhi ya kutahiniwa sawa na masomo mengine.
Tunaishauri serikali irudishe na kuimarisha Elimu ya Dini Mashuleni( EDIMASHUTA) na kurudisha mitaala iliyokuwepo pamoja na kuruhusu taasisi za dini kupeleka waalimu kwa ajili ya kufundisha somo la dini.
Mpango huu ukitekelezwa utasaidia kuwajengea watoto wetu misingi ya maadili mema ili hatimaye tuwe na taifa lenye viongozi na raia wema. Jambo hili litasaidia kujenga jamii yenye amani na utangamano na kuruhusu mazingira ya kupata ustawi kama taifa.
3:3 Vyanzo vya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu
Katika mpango huu, Chama cha Biblia cha Tanzania kinalenga kupata fedha kutoka:
- Taasisi za kanisa
- Mashirika mbalimbali
- Watu binafsi
Aidha Chama katika nia hii njema kinaomba kuungwa mkono na serikali kwa kushiriki katika kazi ya kuhamasisha taasisi, mashirika na wadau mbalimbali ili waweze kushiriki kuchangia mpango huu.
3.4 Kiasi cha fedha, idadi ya Biblia na mgawanyo kwa makundi lengwa
Katika awamu hii ya kwanza Chama cha Biblia kimelenga kuomba kuchangiwa kiasi cha shilingi 10,200,000,000 ambazo zitatumika kununulia jumla ya Biblia 510,000 ambazo mgao wake kwa makundi lengwa utakuwa kama ifuatavyo:
- Watoto – Biblia laki nne (400,000)
- Vijana – Biblia laki moja (100,000)
- Wafungwa – Biblia elfu kumi (10,000)
Kwa sasa Chama tayari kinayo miswada ya Biblia za makundi lengwa yote yaani watoto, vijana na wafungwa. Biblia hizi zinaweza kuchapishwa na wachapishaji wakati wowote fedha zitakapokuwa zimepatikana.
Malipo yakishafanyika inakadiriwa kuwa kazi ya kuchapa, kusafirisha na kupokelewa inachukua muda wa miezi mitatu hadi minne.
3:5 Mikoa na mgao wa Biblia kwa makundi lengwa.
Zoezi hili ni endelevu, lakini katika awamu hii ya kwanza Chama kimelenga kugawa Biblia kwa watoto, vijana na wafungwa katika mikoa ifuatayo :-
Na |
Mkoa |
Watoto |
Vijana |
Wafungwa |
||
|
Makisio |
Halisi |
Makisio |
Halisi |
Halisi |
|
1. |
Dodoma |
730,000 |
100,000 |
180,000 |
25,000 |
3,000 |
2, |
Mara |
580,000 |
82,000 |
145,000 |
20,500 |
3,000 |
3. |
Manyara |
610,000 |
88,000 |
152,500 |
21,500 |
1,000 |
4. |
Pwani |
470,000 |
66,000 |
117,500 |
16,500 |
1,000 |
5. |
Singida |
470,000 |
66,000 |
117,500 |
16,500 |
2,000 |
Jumla kuu |
2,860,000 |
400,000 |
712,500 |
100,000 |
10,000 |
3:6 Usambazaji wa Biblia kwa makundi lengwa.
3:6:1 Mashule
Biblia zitasambazwa na Chama cha Biblia katika mashule kwa kushirikiana na Maafisa Elimu, Waalimu Wakuu wa Mashule, Viongozi wa Makanisa na Waalimu wa Dini mashuleni.
3:6:2 Magereza
Biblia zitasambazwa katika Magereza kwa kushirikiana na Wakuu wa Magereza na Wachungaji wanaotoa huduma ya kiroho magerezani.
4: 0 MWISHO
Mpango huu una umuhimu wa kipekee katika kipindi hiki ambacho tunashudumia mmomonyoko wa maadili ukienda kasi katika jamiii yetu hasa kwa kundi la watoto na vijana ambalo linatarajia kutoa viongozi wa baadae wa taifa letu.
Tunaomba serikali ituunge mkono katika nia hii njema ya kuwajenga watoto, vijana na wafungwa kiroho. Faida ni kubwa kwa afya ya taifa. Kuchukua hatua sasa ni vizuri.
Addresses
16 Hatibu / 9th Road, Madukani Area.
P.O BOX 175, Dodoma -Tanzania.
Phone
+255 (0) 765 530 892
info@biblesociety-tanzania.org
I HIGHL RECOMMEND THIS BIBLE VERSION.
I HAVE ENJOYED READING IT.
IT IS CLEAR AND SIMPLE TO UNDERSTAND.EL