Uzinduzi wa sehemu ya Biblia za vitabu vya 2 Samweli, Ruthi, na Yona kwa lugha ya Kinyamwezi.
Uzinduzi wa Tafsiri ya Biblia
Hafla ya Uzinduzi
29 Septemba 2024
Hafla ya uzinduzi wa tafsiri ya vitabu vya Biblia kwa lugha ya Kinyamwezi ilifanyika katika kanisa la Moraviani, Parishi ya Ipole. Tukio hili lilihudhuriwa na viongozi wa kanisa, wawakilishi wa Chama cha Biblia cha Tanzania, na watafsiri wa Biblia.
HABARI KAMILI
Chama cha Biblia cha Tanzania kimefanya uzinduzi wa sehemu ya Biblia za vitabu vya 2 Samweli, Ruthi, na Yona kwa lugha ya Kinyamwezi. Uzinduzi huo umefanyika katika kanisa la Moraviani, Parishi ya Ipole, wilayani Skonge, mkoa wa Tabora. Tukio hili limeongozwa na Katibu wa Kanisa wa Wilaya ya Skonge, Mchungaji Jackson Mkombo, mbele ya waumini wa Parishi ya Ipole, chini ya Mchungaji Charles Kavula.
Kwa upande wa Chama cha Biblia cha Tanzania, walihudhuria wawakilishi kadhaa akiwemo Meneja wa Tafsiri wa Chama hicho, Dada Leah Kiloba, pamoja na Mchungaji Samweli Mshana, ambaye ni Meneja wa Mahusiano na Makanisa. Pia, Mwinjiristi Choyo Sabanja alihudhuria kama mwakilishi wa meneja wa Uenezi na Masoko.
Watafsiri wa Biblia walioshiriki katika kazi ya kutafsiri vitabu hivi walikuwepo pia katika hafla hiyo. Wakiwa wameongozwa na Mratibu wao, Mchungaji Christe Katuma wa Kanisa la Moravian Tabora mjini, walihusisha Mchungaji Elack Kadubula wa Kanisa la TAG Ipuli, Tabora, Mchungaji Ellen Mpasi wa Kanisa la Moraviani Skonge Mission, na Mchungaji George Ruvula wa Kanisa la Moraviani Tabora mjini. Mwakilishi wa wahakiki, Mchungaji Festo Karangu wa Kanisa la Pentekoste Ipole, Skonge, Tabora, naye pia alishiriki.
Tafsiri ya Biblia kwa lugha ya Kinyamwezi ilianza mwezi Machi mwaka 2020, na hadi sasa, watafsiri wamefanikiwa kukamilisha vitabu vinne, ambavyo ni 1 Samweli, 2 Samweli, Ruthi, na Yona. Uzinduzi wa vitabu hivi umechochea zaidi jitihada za kuendelea na mchakato wa kutafsiri Biblia nzima kwa lugha ya Kinyamwezi.
Meneja Tafsiri wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Dada Leah Kiloba, alitoa ombi kwa kanisa kuendelea kupitia vitabu vilivyozinduliwa ili kama kuna makosa yoyote, yarekebishwe kabla ya Biblia nzima kukamilika. Lengo ni kuhakikisha kuwa Biblia inatolewa bila makosa yoyote ambayo yanaweza kupotosha maana ya Neno la Mungu.
Mchungaji Samweli Mshana, Meneja wa Mahusiano na Makanisa wa Chama cha Biblia cha Tanzania, aliomba ushirikiano wa kanisa katika kuiunga mkono kazi za Chama cha Biblia kwa michango, maombi, na kuwa wanachama wa Chama cha Biblia. Pia alikumbushia umuhimu wa kuadhimisha Juma la Biblia ili kusaidia kuhakikisha Neno la Mungu linafikia watu wote nchini Tanzania.
Katika hafla hiyo, Mchungaji Mshana aligawa pia Biblia za Mpiga Mbiu (Proclaimer), ambazo ni Biblia zinazoongea kwa lugha ya Kinyamwezi na Kiswahili. Biblia hizi ni muhimu kwa watu wasiojua kusoma na kuandika, au wenye changamoto mbalimbali, ili waweze kusikia na kufahamu Neno la Mungu kwa urahisi zaidi.