
Uzinduzi wa Biblia ya Kihehe
Biblia kwa Lugha ya Kihehe Yazinduliwa Rasmi Iringa – Miaka 30 ya Kazi Yafikia Tamati
Na Mwandishi Wetu, Iringa
29 Juni 2025

Dr. Alfred Elias Kimonge akikabidhi Biblia kwa ajili ya kuzinduliwa.
Mgeni rasmi.
Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, ambaye alikipongeza Chama cha Biblia cha Tanzania (CBT) kwa kazi kubwa na ya kipekee ya kutafsiri Neno la Mungu katika lugha mbalimbali za makabila nchini. ‘‘Biblia hii ni zawadi kubwa kwa jamii ya Wahehe na kizazi kijacho. Nitalitunza Neno hili takatifu, na kila siku nitaanza siku yangu nikiwa nimesoma Biblia hii kwa lugha ya mama yangu,” alisema Mhe. Lukuvi.

Mhe. William Vangimembe Lukuvi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), akihutubia.
Biblia iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kihehe imezinduliwa rasmi leo katika ibada maalum iliyofanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme, Anglikana Iringa Mjini, mkoani Iringa, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, makanisa na jamii ya Wahehe kwa ujumla.

Askofu Joseph Mwenyekiti wa CCT Mkoa Iringa na Askofu Anglican Dayosisi ya Ruaha akifanya uzinduzi wa Biblia ya Kihehe.



Dkt. Alfred Elias Kimonge akizungumza kabla ya kukabidhi Biblia ya Kihehe ili izinduliwe.

Safari ya Miaka 30
Kwa mujibu wa Dkt. Alfred Elias Kimonge, Katibu Mkuu wa CBT, mchakato wa kutafsiri Biblia hiyo ulianza mwaka 1994 baada ya maombi kutoka kwa Makanisa ya Iringa. Mradi huo ulisimamiwa na Chama cha Biblia Tanzania kwa kushirikiana na makanisa mbalimbali, wataalamu wa lugha, wahakiki, watafsiri, na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Kimonge alibainisha kuwa tafsiri ya Agano Jipya ilikamilika mwaka 2004 na kuzinduliwa rasmi mwaka 2008. Tafsiri ya Agano la Kale ilianza mwaka 2009, na sasa Biblia kamili imekamilika na kuzinduliwa rasmi leo tarehe 29 Juni, 2025. ‘‘Biblia inayozinduliwa leo inapatikana katika matoleo mawili: toleo la Kiprotestanti lenye vitabu 66, na toleo lenye vitabu 72 lijulikanalo kama Deuterokanoni, linalofaa zaidi kwa matumizi ya Makanisa ya Kikatoliki (TEC),” aliongeza kusema.
‘‘Tunamshukuru Mungu kwa kuona siku hii. Hii ni ushuhuda wa kuwa Neno la Mungu linaweza kufika katika kila lugha, kwa kila mtu,” alihitimisha Dkt. Kimonge.
Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Iringa
Mhe Justin Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo akitoa salaam za furaha Kwa kupata Biblia hiyo uku akisifu juhudi za watafsiri, wahariri, na wadau wa kiimani kwa kazi hii kubwa.


Mhe Justin Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo.
Risala na Maombi Maalum
Katika risala iliyosomwa kwa niaba ya Kamati ya Uzinduzi, viongozi wa makanisa na jamii walitoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusaidia katika masuala yafuatayo:
- Kutambua Biblia ya Kihehe kama waraka rasmi wa lugha ya Kihehe
- Kuandaliwa kwa Kamusi ya Biblia ya Kihehe
- Kutolewa kwa Biblia ya Kihehe kwa njia ya sauti (Audio Bible)
- Kuwepo kwa Biblia ya Kihehe katika mfumo wa mtandaoni
- Kuhifadhi Biblia hiyo katika Maktaba na Makumbusho ya Taifa



Ushiriki wa Viongozi na Jamii
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na maaskofu kutoka madhehebu mbalimbali, wawakilishi wa serikali, wabunge, viongozi wa mila na mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Iringa.
Miongoni mwa viongozi wa dini waliokuwepo ni pamoja na:
- Askofu Dkt. Blaston Gaville (KKKT – Iringa)
- Askofu Dkt. Joseph Mgomi (Anglikana – Ruaha)
- Mhashamu Romanus Mihali (RC – Iringa)
- Askofu Prof. Mdegella, Askofu Mtetemela, na Askofu Ngalalekumtwa






Kumbukizi za Watafsiri
Shukrani na heshima zilitolewa kwa watafsiri na wahakiki waliotoa mchango mkubwa, lakini hawakuweza kushuhudia uzinduzi huu, akiwemo:
- Marehemu Mch. Lambert Mtatifikolo
- Marehemu Mwl. Evaristo Mahimbi
- Marehemu Mch. Israeli Kiponda
Hitimisho na Maono ya Baadaye
Biblia hii inatarajiwa kusaidia jamii ya Kihehe kusoma, kuelewa, na kuishi Neno la Mungu kwa undani zaidi katika lugha yao ya moyo. Viongozi walisisitiza kuwa kazi ya Mungu kupitia tafsiri ya Biblia inapaswa kuungwa mkono zaidi, ili kufanikisha tafsiri katika lugha nyingine za makabila ya Tanzania.


