MAHAFALI YA WAHITIMU WA CHIBWEDA MAGUBIKE TAREHE 19/09/2020.
LWA Kikagulu wahitimu 248 waliomaliza na kufaulu mafunzo ya kusoma na kuandika katika awamu ya pili ya mahafali ambayo yalikuwa yafanyike tarehe 21/03/2020 lakini yakahirishwa kutokana na covid -19. Sasa yalifanyika tarehe 19/09/2020 katika Kanisa la Anglikana huko Magubike.
Mratibu wa mpango huu Mwl. Frank Makalla wa kwanza kushoto kwa waliokaa mbele akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu waliosimama nyuma wenye vyeti pamoja na mgeni rasmi Canon Elias Lucas Chamwenye wa tatu kutoka kushoto na wageni wengine walioalikwa kwenye mahafari hayo.
Awamu ya kwanza waliohitimu ni jumla ya watu 69 ambapo wanawake ni 56 na wanaume ni 13 kutoka vijiji 5 Gairo ambavyo ni Gairo, Mogohigwa, Tabuhoteli, Mtumbatu pamoja na Kibedya.
Awamu ya pili waliohitimu jumla ni 248 ambapo wanawake ni 214 na wanaume ni 34; kutoka kwenye vijiji 13 ambavyo ni Magubike, Nguyami, Berega, Chakwale, Ibindo, Mwandi, Mamboya, Mbili, Dumbaalume, Maguha, Magela, Kiegeya Pamoja Na Mabula.
Waliojiandikisha ni 423 kati yao waliohitimu ni 317 na ambao hawajahitimu ni 106 kutokana na changamoto mbalimbali kama vile kuhama, shughuli za mashamba ,na matatizo mbalimbali ya kijamii.
Akizungumza jana baada ya kukabidhi vyeti kwa awamu ya pili ya wahitimu hao, Mratibu wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Mwl.Frank Makalla alisema wahitimu hao ni wa awamu ya pili ya programu iliyolenga kuwajengea uwezo wa kusoma na kuandika watu wazima wanaoanzia miaka 14 na kuendelea.
Mratibu wa Chama cha Biblia Tanzania, Mwl.Frank Makalla akizungumza na wahitimu wa awamu ya pili katika mahafali hayo huku akiwasisitiza wasiache kufanya yale waliyofundishwa pia wahakikishe kuwa kupitia wao watu wengi zaidi walijue neno la Mungu.
Mratibu wa mpango wa elimu kwa watu wazima kutoka Chama Cha Biblia Cha Tanzania akiongea jambo katika mahafali ya awamu ya pili iliyofanyika Magubike. Alisema kuwa mahafali hayo ni mwendelezo wa mahafali ya awamu ya kwanza ya program hiyo iliyoanza mwaka 2017, ambapo watu 120 walijiandikisha huku watu 97 walihitimu mafunzo hayo ambayo pamoja na kuwafundisha kwa kutumia lugha ya chikagulu kufundishia, mafunzo hayo yanafanywa pia kuweza kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili.
Programu hiyo inafadhiliwa na Chama cha Biblia cha Finland, Chama cha Biblia cha Tanzania pamoja na Summer Institute of linguistics (SIL) ambao wanatoa utaalamu wa waalimu pamoja na mwongozo wa kuandaa vitabu vya kufundishia. Programu hiyo inalenga zaidi kuwainua wanawake kujifunza kusoma na kuandika ingawa na wanaume wanakaribishwa kushiriki.
Wahitimu wa CHIBWEDA wakiwa katika picha ya pamoja katika mahafali yao iliyofanyika mnamo tarehe 19/09/2020 huko Magubike siku ya Jumamosi.
Mratibu wa mpango huu Mwl. Makalla alisema kati ya watu wazima 248 waliohitimu, wanawake ni 214 na wanaume ni 34 katika awamu hii ya pili ambao walishindwa kufanya hivyo mwezi wa Machi 2020 kutokana na ugonjwa wa corona ulioikumba Dunia nzima wakati huo. Akizungumzia sababu ya baadhi ya watu waliojiandikisha kushindwa kumaliza, Mwl. Makallla alisema kwa wale walioacha masomo, hao wamepewe nafasi ya kujiunga na darasa la awamu ya tatu ambalo limeanza tayari wakiendelea na mafunzo. Aidha, Mwl. Makalla aliomba ushirikiano na serikali katika mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwafanya wananchi waliokosa fursa ya kusoma na kuandika kujiunga na kuendelea kupata elimu hiyo.
“Katika programu yetu hii tumekuwa tukichukua wale wenye umri wa kuanzia miaka 14 na kuendelea, hivyo wale wenye miaka 14 hadi 17, serikali inaweza kuwatambua na kuwaingiza katika mfumo wa MEMKWA katika shule za msingi kama ambavyo Serikali inaelekeza kupitia wizara ya Elimu ili wakajifunze zaidi kwa sababu sisi hapa tunawafundisha kusoma na kuandika tu huko watajifunza masomo mengine pia kama Hesabu, Sayansi, Jiografia Historia na kadhalika.
Mgeni rasmi kabla ya kutoa vyeti kwa kundi la pili la wahitimu wa Chibweda ‘Furaha’ Canon Elias Lucas Chamwenye ambae alimwakilisha Askofu Godfrey Sehaba wa dayosisi ya Morogoro Kanisa la Anglikana aliwataka wahitimu hao kutumia maarifa hayo kujiendeleza kiuchumi na kushiriki katika uchumi wa taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kutumia haki yao ya kimsingi ya kupiga kura kuwachagua viongozi wa nchi Raisi, Wabunge, na Madiwani ifikapo tarehe 28/10/2020.
Mgeni rasmi; Canon Elias Lucas Chamwenye akiwa anazungumza na wahitimu wa awamu ya pili katika mahafali hayo.
Naye Meneja wa Miradi na utunishaji mfuko wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Mch. Samwueli Mshana ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania Ndg. Alfred Elias Kimonge, alisema lengo la Chama cha Biblia ni kutafsiri Biblia kwa lugha za asili, kukuza na kutunza lugha ya asili lakini pia kusaidia jamii husika kusoma na kuelewa Neno la Mungu.
Meneja wa miradi na utunishaji mfuko wa Chama cha Biblia cha Tanzania Mch. Samwueli Mshana akiwapongeza wahitimu wa mahafali ya pili.
Katibu wa idara ya mamaendeleo ya Akina Mama UMAKI Josephine Semwenda katika Dayosisi ya Morogoro ambaye alialikwa kuwatia moyo wahitimu hao aliwasisitizia wahitimu kutokuogopa kuitangaza lugha ya Chikagulu kila mahali katika eneo lao la ukaguruni na kuwahimiza kuwa mabalozi wema katika kuilinda lugha yao isipotee, alitumia nafasi hiyo pia kuwapongeza. wahitimu wote na kuwatakia kila lakheri katika kutekeleza majukumu ya kijamii na Kanisa.
Katibu wa UMAKI Ndg. Josephine Semwenda akitoa wosia wake kwa wahitimu kuzidi kutia juhudi katika kuwafundisha wengine hususani neno la Mungu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nguyami Mh.Gilbert Ngiga ambaye alitembea umbali mrefu kuja kushuhudia mahafali hayo alisema wao katika kijiji chao tayari wameshamchukua moja kati ya wahitimu hawa anayeitwa Rehema Penford na kumuweka katika kamati ya maendeleo ya kijiji, na wataendelea kufanya hivyo ili kuwahamasisha wengine kujiunga na mpango huu mzuri.
Mwenyekiti huyo wa kijiji cha Nguyani Mh. Gilbert Ngiga alitoa shukurani zake nyingi kwa Chama cha Biblia chaTanzania kwa juhudi wanazozifanya kuwafikia watu mbalimbaliu.
Katika mahafali hiyo kulikuwa na vikundi mbalimbali vya nyimbo, ngonjera, mashairi, maigizo, na kusoma hadithi kutoka katika kitabu cha Chibweda mbele ya mgeni rasmi.
Kikundi cha nyimbo na ngoma.Kikundi cha wahitimu wakisoma risala.Pichani, ni wahitimu wa awamu ya pili, katika igizo lao wakionyesha madhara ya kutokujua kusoma na kuandika ambapo tunaona mtoto aliyelala hapo chini alipoteza maisha baada ya mama yake kumpa dawa kinyume na maelekezo aliyopewa na daktari. Hii ni kwa sababu mama yake alipopewa taarifa na wenzake kwenda kujiunga na darasa la CHIBWEDA hakuwa tayari kujiunga na elimu ya watu wazima ambayo hutolewa bure na Chama cha Biblia cha Tanzania na kusababisha kifo cha mwanae kwa uzembe.
Katika mahafari hayo yaliyofanyika kanisani Anglikana Magubike na mwenyeji wetu Kasisi Elkana Chogohe wa kanisa hilo. Alitoa shukurani zake kwa wahitimu na waanzilishi wa mafunzo kutoka Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kwa watu wazima waeneo hili la wakagulu.
Kasisi Elkana Chogohe wa kanisa la Anglikana Magubike akitoa shukurani zake kwa wahitimu na waanzilishi wa mafunzo kutoka Chama cha Biblia cha Tanzaniakwa kwa watu wazima waeneo hili la wakagulu.
WAKATI Chama cha Biblia cha Tanzania kikiwa kimetoa msaada wa Biblia Takatifu kwa wafungwa na mahabusu ya Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko yote ya jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Gereza la Segerea, SSP. Daniel Mwakyoma amesema ukosefu wa uzio na upungufu wa nyumba za watumishi ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili gereza hilo.
Makabidhiano ya msaada huo upande wa Gereza la Segerea yamefanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Arch. Ng’wilabuzu Ludigija na Maafisa Waandamizi wa gereza hilo, huku upande wa Chama cha Biblia kikiwakilishwa na wajumbe mbalimbali akiwemo Katibu wa Chama hicho, Mch. Alfred Kimonge, Meneja wa Mahusiano ya Makanisa na Utunishaji wa mfuko wa chama hicho, Mch.Samwel Mshana huku Kanisa Katoliki likiwakilishwa na Mjumbe wa Bodi wa Chama hicho hicho, Padri Chesco Msaga, CPP.S ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo ulioenda sambamba na utoaji wa mahitaji ya kimwili kwa wafungwa na mahabusu hao, unaojumuisha sabauni na dawa ya meno, Katibu wa Chama hicho, Mch. Kimonge amesema, lengo ni kuwapa wahusika fursa ya kusoma Neno la Mungu, linalobadilisha, na kutia faraja, msaada uliopokelewa kwa furaha na wahusika.
“Chama cha Biblia Tanzania ambacho kinajumuisha wanachama kutoka madehebu ya Waprotestanti, Wasabato, Wapentekoste na Wakatoliki, kinaguswa na maisha ya makundi mbalimbali wakiwemo mahabusu na wafungwa kama nyie, hivyo Biblia hizi tunazokabidhi kwenu tunaomba ziwasaidie kufanyie rejea yale mnayohubiriwa…zinafaa hata kwa wale wasiokuwa Wakristo,” amesisitiza.
Msaada huo umeenda sambamba na ziara maalum ya Mkuu mpya wa Wilaya ya Ilala, Arch, Ng’wilabuzu Ludigija kutembela magereza yaliyopo wilayani kwake ya Segerea na Ukonga, kama sehehemu ya kujitambulisha.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Wilaya na wajumbe wa Chama cha Biblia, walipata fursa na kuzungumza na uongozi wa gereza hilo pamoja na kukutana na mahabusu na wafungwa, wakiwemo wanawake na wanaume ambapo waliwasilisha changamoto zao.
Upande wake SSP Mwakoyoma amesema ngome (gereza), haijazungushiwa uzio, hali inayosababisha hali ya usalama kuwa hatarini, hali inayoenda sambamba na ukosefu wa nyumba za watumishi kiasi cha kusababisha asilimi 90 kuishi uraiani nje ya kituo chao cha kazi.
Changamoto nyingine kama zilivyobainishwa na Mkuu huyo wa Gereza ni ukosefu wa huduma ya usafiri kwa mahabusu pindi wanapotakiwa kupelekwa mahakamani kusikiliza kesi zao, uhaba wa maji na kutokuwa na jenereta (standby generator) pindi umeme unapokatika, jambo ambalo ni hatari kwa jumuiya yenye msongamano wa watu kwani pia kuna mlundikano wa mahabusu.
Akitoa kero zinazowakabili wafungwa na mahabusu wanawake, nyampala wa kundi hilo, (jina tunalihifadhi) amesema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni baadhi ya watuhumiwa kuchanganyikiwa kiakili, hali inayosababishwa na masuala mbalimbali likiwemo la kesi zao kutokusikilizwa kwa wakati, jambo ambalo amesema ni hatari kwa wafungwa na mahabusu wengine.
“Kuathirika kisaikolojia… anapiga mahabusu wenzake na anaweza hata kuwafanyia vitendo vingine vya kikatili zaidi, hivyo tunaomba hili liangaliwe na kufikishwa kunakostahili ili ikiwezekana hata wafanyiwe vipimo vya kitaalam zaidi na ikibainika ni shida, basi wapelekwe kwenye magereza yaliyotengwa kwa watu wa namna hii,” amesema.
Changamoto nyingine kwa wanawake ni uhaba wa magodoro hali inayowalazimu baadhi yao kulala chini kwenye sakafu, uhaba wa sare kwa wale ambao tayari wameshahukumiwa, lishe duni kwa watoto wanaoishi na mama zao gerezani pamoja na uhaba wa maji na vifaa vya usafi vya kutosha hali inayosababisha wengi kupata ugonjwa wa UTI.
Asia Mhamed ambaye ni mahabusu Na.125/2016 yeye amesema changamoto zaidi ipo kwa watuhumiwa wa kesi za mauaji, utakatishaji pesa na dawa za kulevya, ambapo amedai zimekuwa hazikilizwi kwa kile wanachoambiwa na mahakimu na majaji wanaosikiliza kesi hizo kuwa wanaendelea na upepelezi na hata wakati mwingine kudai kwamba kesi hizo uendeshaji wake unahitaji hela ambayo lazima iwe imetengwa kwenye bajeti ya serikali.
Upande wa mahabusu na wafungwa wanaume, mwakilishi wa kundi hilo, Florian Apolynal yeye amesema licha ya baadhi ya watuhumiwa wakiwemo wale wanaokabiliwa na kesi za Uhujumu Uchumi kutekeleza agizo la Rais, la kuandika barua na kutaka kufanyike maelewano (bargaining), lakini hawajui kinachoendelea baada ya kutekeleza hilo.
Pia wamedai kuwa kuna changamoto ya kubambikiziwa kesi zikiwemo za mauaji “… wakishakukamata wanakupa adhabu kali zenye mateso ili wakubadilishia kosa ambalo haujafanya… hivyo wengi humu tuna machungu kwani unakamatwa na kosa la wizi (robbery), lakini kwenye faili unaandikiwa mauji,” amesema mahabusu Charles Raphael Mkanya.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kero hizo amezipelekea na atazifikisha ofisini kwake ajadiliane na wataalam na kile kitakachoshindikana atakipeleka ngazi za juu zaidi ili zipatiwe ufumbuzi.
Watu wazima 317 kati ya 423 kutoka vijiji 20 wameitimu mafunzo ya kusoma na kuandika kwa lugha ya Chikagulu.
Akizungumza jana baada ya kukabidhi vyeti 89 kwa awamu ya kwanza ya wahitimu hao, Mratibu wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Frank Makalla alisema wahitimu hao ni wa awamu ya pili ya programu iliyolenga kuwajenga uwezo wa kusoma na kuandika watu wazima wanaoanzia miaka 15 na kuendelea.
Mratibu wa Mradi Mwl. Frank Makalla
Mratibu wa mpango wa elimu kwa watu wazima kutoka Chama Cha Biblia Cha Tanzania akiongea jambo katika mahafali ya awamu ya pili iliyofanyika GairoAwamu ya kwanza ya programu hiyo iliyoanza mwaka 2017, watu 120 walijiandikisha huku watu 97 walihitimu mafunzo hayo ambayo pamoja na kuwafundisha kwa lugha ya Chikagulu, mafunzo hayo yanafanywa pia kuweza kusoma na kuandika kwa Kiswahili.
Programu hiyo inafadhiliwa na Chama cha Biblia cha Tanzania, Chama cha Biblia cha Finland na Taasisi ya Lugha ya Kenya, pia unalenga zaidi kuwainua wanawake ingawa na wanaume wanaruhusiwa kushiriki.
Makallla alisema kati ya watu wazima 317 waliohitimu, wanawake ni 270 na wanaume ni 47.
Akizungumzia sababu ya baadhi ya watu waliojiandikisha kushindwa kumaliza, Makallla alisema kwa wale walioacha masomo, hao wamepewe nafasi ya kuingia darasa la awamu ya tatu linalotarajia kuanzia Mei 15, mwaka huu ikiwa ni baada ya walimu kupewa mafunzo ya kujengewa uwezo.
Aidha, Makalla aliomba ushirikiano na serikali katika mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwafanya wananchi waliokosa fursa ya kusoma na kuandika.
“Katika programu yetu tumekuwa tunachukua wale wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea, hivyo wale wenye miaka 15 hadi 17, serikali inaweza kuwatambua na kuwaingiza katika mfumo wa MEMKWA ili wakajifunze Zaidi kwa sababu sisi hapa tunawafundisha kusoma na kuandika tu, ” alieleza.
Mgeni rasmi Dk. Jackson Nyanda (Makamu Mwenyekiti Chama cha Biblia cha Tanzania)
Kabla ya kutoa vyeti kwa kundi la kwanza la wahitimu wa 89 wa Chibweda ‘Furaha’ Dk Jackson Nyanda aliwataka wahitimu hao kutumia maarifa hayo kujiendeleza kiuchumi na kushiriki katika uchumi wa taifa kwa ujumla.
Meneja Miradi na Uhusiano wa Makanisa Mch. Samwueli Mshana
Naye Meneja wa Miradi na utunishaji mfuko wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Samwueli Mshana ambaye pia alimwakilisha Katibu wa chama hicho, alisema lengo la chama chake ni kutafsiri Biblia kwa lugha za asili, kukuza na kutunza lugha ya asili lakini pia kusaidia jamii husika kuelewa Neno la Mungu.
Na. Ndugu Frank Makalla (Msimamizi Mkuu wa Mradi-CBT).
Chama Cha Biblia Cha Tanzania kilianzisha kisomo cha elimu ya watu wazima kwa kushirikiana na Chama Cha Biblia Cha Finland na SIL (Summer Institute of linguistic) mnamo mwaka 2017 na mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa kuandaa vitabu kwa ajili ya wanakisomo wa elimu ya watu wazima katika msemo wa Kikagulu na kanisa katika eneo hilo lilishiriki kikamilifu kwa kutoa watafsiri na waandishi. Ndipo mradi ukaanza 2018 ukiwa na walimu 20 (ishirini). Walimu hao walianza na wanafunzi mia ishirini ambavyo wanafunzi 97 walihitimu na kupewa vyeti mwezi machi 2019.
Na baada ya hapo Madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika yalianza mwezi wa nane 2019 katika vijiji 20 (ishirini) vingine na kila kijiji kina darasa moja na kila darasa lina walimu wawili 2 (wawili) na jumla ya wanafunzi ni 423 kwa vijiji vyote.
Madarasa hayo ishirini yanaendelea vizuri katika kiwango cha 97% (asilimia tisini na saba) wanaweza kusoma na kuandika. Tunatarajia watahitimu mwisho wa mwezi huu wa February 2020 na mahafali yatakuwa mwezi wa tatu kuanzia tarehe 14/03/2020 (kumi na nne), 21/03/2020 (ishirini na moja) na 28/03/2020 (ishirini na nane) kwa maana yamegawanywa kwenye vituo vitatu ambavyo ni Gairo, Nguyami na Magubike.
Darasa la Chibweda kijiji cha Kibedya
Mwalimu Devotha Madihi wa darasa la Chibweda kijiji cha Kibedya akifundisha darasani. Darasa hili lina mama mmoja mwenye watoto mapacha wanaonekana hapo chini na amekuwa akihudhulia vizuri sana darasani.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Berega
Wanakisomo wa darasa la Kikagulu katika Kijiji cha Berega wanajifunza kusoma na kuandika kwa kutumia lugha ya Kikaguru wakifundishwa na waalimu wao Rose Chitemo mwenye kilemba na Sofia Muhumba.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Berega
Mwanafunzi Merina Malali wa Darasa la Chibweda Berega akiwa anaandika kufuatia maelekezo ya waalimu.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Kiegea
Darasa la Kiegea wanafatilia mafundisho ya mwalimu ubaoni.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Tabuhoteri
Darasa la kijiji cha Tabuhoteli lina wakina mama wenye umri mkubwa na wana bidii sana katika kujifunza kusoma na kuandika.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Ibindo
Wanakisomo katika kijiji cha Ibindo wakipata maelekezo kutoka kwa walimu wao kuhusu kusoma na kuandika.
Kujifunza kuandika
Mwanafunzi Merina Malali wa Darasa la Chibweda (mwenye kilemba cha pink) katika kijiji cha Berega akiwa anaandika kufuatia maelekezo ya waalimu.
Wanakisomo awa, wapo katika marudio wakisubiri kupewa mitihani yao ya mwisho ili hatimaye kukabidhiwa vyeti kwa wale watakaofaulu na kuhitimu masomo yao vizuri.
CHANGAMOTO:
Kwa kuwa hawa ni watu wazima zipo changamoto mbali mbali zinazoathiri mahudhurio darasani kama vile:- kazi za shamba, misiba kijijini na nje ya kijiji, kuumwa, kuuguliwa, mito kujaa na kuwatenganisha kwa muda, kutomaliza silabasi yao kwa wakati kwa kuwa wapo wenye kujifunza kwa polepole kulingana na umri wao na kusababisha waalimu kuwa fuatilia na kuwaelekeza kwa muda zaidi. n.k.
Changamoto katika kuwafikia
Wakati mwingine kuna changamoto ya kuwafikia wanakisomo kwa sababu ya ubovu wa miundombinu hasa barabara kama picha inavyoonesha hapa chini.
Kunasua gari
Wakati mwingine kipindi cha mvua changamoto kubwa ni barabara, mfano picha hiyo hapo Gari lilikwama kwenye matope kutokana ubovu wa barabara wakati tunakwenda kuona darasa la Mtumbatu na tulisaidiwa na wanakijiji kulinasua gari kwenye matope (Ndugu Frank Makalla akieleza).
Kutokana na kikao cha mapitio ya maendeleo ya mradi wa tafsiri ya Biblia kwa Lugha ya Kirimi November 04-09, 2019, Mkoani Singida, Tafsri bingwa Dr.Samy Tioye kutoka UBS athibitisha mradi huu kuendelea vizuri na umefikia hatua nzuri zaidi kwa hali hiyo Biblia ya Lugha ya Kirimi tunaitegemea iwe imekamilika 2020 December.
Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kushirikiana na Kanisa tunafanya kazi ya kutafsiri Biblia kwa Lugha ya Kirimi. Kazi hii inafanyika kwa ustadi mkubwa na kuzingatia kanuni na utalaam wa tafsiri ya Biblia kutoka muungano wa vyama vya Biblia Ulimwenguni (UBS).
Kwa mantiki hiyo hapa chini katika picha tunaona Dr.Samy Tioye mmoja wa watafsiri Bingwa wa Lugha kutoka UBS akiwa na watafsiri wa Lugha ya Kirimi katika kuangalia usahihi wa kazi hii muhimu.
Kirimi team, Singida, Tanzania
Mshauri bingwa wa Tafsiri za Biblia Dr.Samy Tioye akiwa anawaonyesha aina mbalimbali za tafsiri za Biblia na namna zinavyoweza kutumika kusaidia tafsiri ya Biblia kwa Lugha ya Kirimi, Katika ofisi ya tafsiri ya Biblia kwa Lugha Kirimi Mkoani Singida.
Maelekezo
Mshauri bingwa wa Tafsiri za Biblia Dr.Samy Tioye akiwa anaelezea jambo kwa watafsiri wa Biblia kwa Lugha ya Kirimi, Katika ofisi ya tafsiri ya Biblia kwa Lugha Kirimi Mkoani Singida.
Umakini
Watafsiri wa Biblia kwa Lugha ya Kirimi (Mch. Elia Mande na Mch. Simoni Kusina) wakipitia na kufanya masahihisho ya kitabu cha Kumbukumbu la torati.
kusaiisha
Mrs. Joyce Shisha, Katibu muhutasi wa mradi wa Kirimi akiingiza masahihisho ya kitabu cha Kumbukumbu ya tarati kwenye Programu maalumu ya Tafsiri za Biblia iitwayo Paratext.
Pamoja
Picha ya pamoja kati ya Meneja wa Tafsiri, mtafsiri Bingwa pamoja na watafsiri wa Biblia kwa Lugha ya Kirimi.