IMG 20200831 WA0009Na Dalphina Rubyema

WAKATI Chama cha Biblia cha Tanzania kikiwa kimetoa msaada wa Biblia Takatifu kwa wafungwa na mahabusu ya Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko yote ya jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Gereza la Segerea, SSP. Daniel Mwakyoma amesema ukosefu wa uzio na upungufu wa nyumba za watumishi ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili gereza hilo.

IMG 20200829 WA0013

Makabidhiano ya msaada huo upande wa Gereza la Segerea yamefanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Arch. Ng’wilabuzu Ludigija na Maafisa Waandamizi wa gereza hilo, huku upande wa Chama cha Biblia kikiwakilishwa na wajumbe mbalimbali akiwemo Katibu wa Chama hicho, Mch. Alfred Kimonge, Meneja wa Mahusiano ya Makanisa na Utunishaji wa mfuko wa chama hicho, Mch.Samwel Mshana huku Kanisa Katoliki likiwakilishwa na Mjumbe wa Bodi wa Chama hicho hicho, Padri Chesco Msaga, CPP.S ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo ulioenda sambamba na utoaji wa mahitaji ya kimwili kwa wafungwa na mahabusu hao, unaojumuisha sabauni na dawa ya meno, Katibu wa Chama hicho, Mch. Kimonge amesema, lengo ni kuwapa wahusika fursa ya kusoma Neno la Mungu, linalobadilisha, na kutia faraja, msaada uliopokelewa kwa furaha na wahusika.

“Chama cha Biblia Tanzania ambacho kinajumuisha wanachama kutoka madehebu ya Waprotestanti, Wasabato, Wapentekoste na Wakatoliki, kinaguswa na maisha ya makundi mbalimbali wakiwemo mahabusu na wafungwa kama nyie, hivyo Biblia hizi tunazokabidhi kwenu tunaomba ziwasaidie kufanyie rejea yale mnayohubiriwa…zinafaa hata kwa wale wasiokuwa Wakristo,” amesisitiza.

IMG 20200829 WA0015

Msaada huo umeenda sambamba na ziara maalum ya Mkuu mpya wa Wilaya ya Ilala, Arch, Ng’wilabuzu Ludigija kutembela magereza yaliyopo wilayani kwake ya Segerea na Ukonga, kama sehehemu ya kujitambulisha.

Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Wilaya na wajumbe wa Chama cha Biblia, walipata fursa na kuzungumza na uongozi wa gereza hilo pamoja na kukutana na mahabusu na wafungwa, wakiwemo wanawake na wanaume ambapo waliwasilisha changamoto zao.

Upande wake SSP Mwakoyoma amesema ngome (gereza), haijazungushiwa uzio, hali inayosababisha hali ya usalama kuwa hatarini, hali inayoenda sambamba na ukosefu wa nyumba za watumishi kiasi cha kusababisha asilimi 90 kuishi uraiani nje ya kituo chao cha kazi.

Changamoto nyingine kama zilivyobainishwa na Mkuu huyo wa Gereza ni ukosefu wa huduma ya usafiri kwa mahabusu pindi wanapotakiwa kupelekwa mahakamani kusikiliza kesi zao, uhaba wa maji na kutokuwa na jenereta (standby generator) pindi umeme unapokatika, jambo ambalo ni hatari kwa jumuiya yenye msongamano wa watu kwani pia kuna mlundikano wa mahabusu.

Akitoa kero zinazowakabili wafungwa na mahabusu wanawake, nyampala wa kundi hilo, (jina tunalihifadhi) amesema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni baadhi ya watuhumiwa kuchanganyikiwa kiakili, hali inayosababishwa na masuala mbalimbali likiwemo la kesi zao kutokusikilizwa kwa wakati, jambo ambalo amesema ni hatari kwa wafungwa na mahabusu wengine.

IMG 20200829 WA0012

“Kuathirika kisaikolojia… anapiga mahabusu wenzake na anaweza hata kuwafanyia vitendo vingine vya kikatili zaidi, hivyo tunaomba hili liangaliwe na kufikishwa kunakostahili ili ikiwezekana hata wafanyiwe vipimo vya kitaalam zaidi na ikibainika ni shida, basi wapelekwe kwenye magereza yaliyotengwa kwa watu wa namna hii,” amesema.

Changamoto nyingine kwa wanawake ni uhaba wa magodoro hali inayowalazimu baadhi yao kulala chini kwenye sakafu, uhaba wa sare kwa wale ambao tayari wameshahukumiwa, lishe duni kwa watoto wanaoishi na mama zao gerezani pamoja na uhaba wa maji na vifaa vya usafi vya kutosha hali inayosababisha wengi kupata ugonjwa wa UTI.IMG 20200829 WA0016

Asia Mhamed ambaye ni mahabusu Na.125/2016 yeye amesema changamoto zaidi ipo kwa watuhumiwa wa kesi za mauaji, utakatishaji pesa na dawa za kulevya, ambapo amedai zimekuwa hazikilizwi kwa kile wanachoambiwa na mahakimu na majaji wanaosikiliza kesi hizo kuwa wanaendelea na upepelezi na hata wakati mwingine kudai kwamba kesi hizo uendeshaji wake unahitaji hela ambayo lazima iwe imetengwa kwenye bajeti ya serikali.

Upande wa mahabusu na wafungwa wanaume, mwakilishi wa kundi hilo, Florian Apolynal yeye amesema licha ya baadhi ya watuhumiwa wakiwemo wale wanaokabiliwa na kesi za Uhujumu Uchumi kutekeleza agizo la Rais, la kuandika barua na kutaka kufanyike maelewano (bargaining), lakini hawajui kinachoendelea baada ya kutekeleza hilo.

Pia wamedai kuwa kuna changamoto ya kubambikiziwa kesi zikiwemo za mauaji “… wakishakukamata wanakupa adhabu kali zenye mateso ili wakubadilishia kosa ambalo haujafanya… hivyo wengi humu tuna machungu kwani unakamatwa na kosa la wizi (robbery), lakini kwenye faili unaandikiwa mauji,” amesema mahabusu Charles Raphael Mkanya.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kero hizo amezipelekea na atazifikisha ofisini kwake ajadiliane na wataalam na kile kitakachoshindikana atakipeleka ngazi za juu zaidi ili zipatiwe ufumbuzi.

× How can I help you?