CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA NA PROGRAMU YA BIBLIA MAGEREZANI
ZIARA KATIKA MAGEREZA YA MSALATO NA KONGWA DODOMA
Moja kati ya wajibu muhimu kwa Chama cha Biblia cha Tanzania ni kuhakikisha kuwa watu wote wanapata fursa ya kupata maandiko matakatifu. Kutokana na jukukumu hilo tarehe 27/11/2018 watumishi wa Idara ya Mahusiano na baadhi ya Wale wa Mawasiliano, walipata nafasi ya kutembelea Gereza la Msalato Dodoma na kugawa Biblia, Sabuni na dawa ya meno kwa Wafungwa wa gereza hilo la Msalato. Mkuu wa Gezea la Msalato Afande Huruma Mwakaji akishirikiana na Msaidizi wake na Maafande wengine walitupokea vizuri sana na kutupa ushirikiano wa hali ya juu.
Meneja Mahusiano wa Chama Cha Biblia Rev. Samweli Mshana akikabidhi Biblia na mahitaji mbalimbali ya wafungwa kwa Mkuu wa Gezea la Msalato Afande Huruma Mwakaji
Picha ya pamoja kati ya Watumishi wa Chama cha Biblia, viongozi wa kanisa la KKKT Dodoma na viongozi wa gereza la Msalato
Jukumu la kugawa Biblia halikuishia Gereza la Msalato tu kwani Tarehe 28/11/2018 Meneja Mahusiano na kikosi kazi chake walipata nafasi ya kutembelea Gereza la Kongwa Dodoma. Katika Gereza hili tulipokelewa vizuri sana na kupewa maelezo ya jinsi Wafungwa wanavyohitaji msaada wa Maandiko na vifaa vingne kwani wanatakiwa kjujitegemea.Chama cha Biblia tulifaulu kugawa Maandiko Matakatifu,sabuni, dawa ya Meno na Taulo za akina Mama.Mkuu wa Gereza Afande Nyonyi alishuru sana Chama cha Biblia cha Tanzania kwa msaada huo kwa Wafungwa.
Meneja Mahusiano wa Chama Cha Biblia Rev. Samweli Mshana akikabidhi Biblia na mahitaji mbalimbali ya wafungwa kwa Mkuu wa Gezea la Kongwa Afande Nyonyi
Picha ya pamoja kati ya Watumishi wa Chama cha Biblia, mkuu wa jimbo wa kanisa la KKKT Kongwa (wa kwanza kulia) na viongozi wa gereza la Kongwa
Hatimaye Biblia ya Kisukuma yazinduliwa kwa kishindo mkoani Mwanza.
Na Felix Jones
Uzinduzi wa Biblia ya Kisukuma umefanyika katika Kanisa Kuu AIC Makongoro Mwanza na kuudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Makanisa mkoa wa Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo Mch. Ipyana Mwangota kwa niaba ya mtafsiri mkuu wa Umoja wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni (UBS), kuwa mchakato wa kutafsiri Biblia kwa lugha ya Kisukuma ulianza miaka thelathini iliyopita. “Tulifanikiwa kutafsiri sehemu ya Biblia kwa lugha kisukuma na kuzinduliwa mwaka 1895 na Mchakato ukaendelea tukapata Agano Jipya mwaka 1925 na baadae kufanyiwa marekebisho na atimaye kuzinduliwa mwaka 2001 na leo tunayofuraha kuzindua au kuweka wakfu Biblia kamili kwa lugha hii ya kisukuma mwaka huu 2021.”
Meneja Tafsri akizungumza kwa niaba ya Mtafsiri Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni (UBS) wakati wa hafla hiyo.
Pamoja na changamoto tulizokabiliwa nazo katika kutafsiri, kuichapisha mpaka leo inazinduliwa, tunakila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kusikia maombi yetu na haja yetu ya moyoni.
Kwa sasa jamii hii ina nafasi ya kumsikiliza Mungu akisema nao kwa lugha yao wenyewe na hivyo historia imejiandika kwa sababu watoto na wajukuu wataitumia Biblia hii kwa miaka mingi na kuienzi lugha yao. Pia ni jambo zuri katika kuihifadhi lugha ya Kisukuma kwa sababu wengi tunafahamu fasihi andishi inahifadhiwa kwa muda mrefu zaidi.
Mara baada ya hotuba hiyo fupi, Mch. Mwangota ndipo alipopata fursa ya kumkabithi Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania Dkt. Alfred Kimonge Biblia hiyo ya Kisukuma ili naye aikabidhi kwa Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande ili iweke wakfu tiyari kwa kutumika katika Kanisa la Mungu.
Mwakilishi wa Translation Consultant (TC) Canon Ipyana Mwangota akimkabidhi Biblia ya Kisukuma Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania Dkt. Alfred Elias Kimonge wakati wa Uzinduzi wa Biblia hiyo ya Kisukuma katika Kanisa la AIC Makongoro Mwanza
Kwa upande wa Katibu Mkuu Dkt. Alfred Kimonge aliomba Biblia hii itumike katika Ibada ili kazi hii iliyofanyika kwa miaka mingi na kwa gharama kubwa isiwe ya bure. Na zaidi aliongeza kuwa kwa niaba ya Chama cha Biblia cha Tanzania ni matumaini yetu kuwa injili ya Wokovu katika Yesu Kristo itawafikia wasukuma katika lugha yao ya moyoni na kusema sasa tumemtambua Mungu anasema na sisi kwa lugha yetu.
Hivyo Wasukuma nao watamsikia Bwana Yesu kwa ukaribu wa moyoni ili wapate fursa ya kushiriki katika halaiki ya mwisho, kama Biblia isemavyo:-
“Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha (Wasukuma)…” (Ufu. 7: 9 – 12).
“Hivyo Ninayoheshima ya kukuomba Baba Askofu Mkuu kuwa uipokee Biblia hii na kuiweka wakfu” alisema Katibu Mkuu wakati wa kukabithi Biblia hiyo ili iwekwe wakfu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania Dkt. Alfred Elias Kimonge akisoma hotuba mbele ya Askofu Mkuu Renatus Nkwande kabla ya kumkabidhi wakati wa Uzinduzi wa Biblia hiyo ya Kisukuma katika Kanisa la AIC Makongoro Mwanza.
Naye Dkt. Alfred Kimonge alipo maliza kusoma hotuba yake ndipo alipopata fursa ya kumkabithi Askofu Mkuu Renatus Nkwande Biblia hiyo ya Kisukuma ili aiweke wakfu tiyari kwa kutumika katika Kanisa la Mungu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania Dkt. Alfred Elias Kimonge akikabidhi Biblia ya Kisukuma kwa Askofu Mkuu Renatus Nkwande wakati wa uzinduzi wa Biblia hiyo ya Kisukuma katika Kanisa la AIC Makongoro Mwanza.
Askofu Mkuu Renatus Nkwande aliipokea kwa furaha kisha akaendelea na taratibu za kuiweka wakfu Biblia hiyo ya Kisukuma.
Askofu Mkuu Renatus Nkwande akisoma sala ya kuzindua hiyo Biblia ya Kisukuma wakati wa sherehe hizo za uzinduzi wa hiyo Biblia ya Kisukuma.
Askofu Mkuu Renatus Nkwande akisaini Biblia ya Kisukuma kuwashilia kupokelewa na Kanisa.
Na hapa ni baadhi ya viongozi na waumini walio weza kuhudhulia katika hafla ya Uzinduzi huo.
Baada ya uzinduzi huo wa Biblia hiyo Baba Askofu na Balozi wa Chama cha Biblia cha Tanzania aliyewakilisha Bodi ya wakurugenzi ya Chama cha Biblia cha Tanzania alipata fursa ya kuhutubia wasukuma waliofika katika uzinduzi huo na pia kutoa salamu kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Chama cha Biblia cha Tanzania na kueleza dhima ya Chama katika mkutadha wa kuakikisha kila Mtu hapa nchini anakuwa na Biblia yake na kwa lugha anayeielewa asa kuwa na Biblia ya moyoni.
Baba Askofu Amos Muhagachi ambaye ni Mwenyekiti msaidizi wa Bodi ya wakurugenzi na Balozi wa Chama cha Biblia akihutubia Kanisa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi.
Kwa upande wa Mgeni rasmi Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande alikipongeza Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kazi nzuri sana ya kuakikisha kila mtu ana Biblia yake na lugha yake na kwa bei mtu anayoweza kuimudu huku akisisitiza Kanisa la Mungu katika kabila la Kisukuma kuhakikisha wanaweka ratiba ya kuwezesha Biblia ya Kisukuma inatumika ili watu weweze kumsikia Mungu akisema nao kwa lugha yao ya Moyoni.
Askofu Mkuu Renatus Nkwande akihutubia Kanisa la Mungu katika Kabila la Wasukuma wakati wa uzinduzi wa Biblia hiyo ya kisukuma.
Pia kinawakaribisha wanachama wote wa Chama cha Biblia walioko mkoa wa Mwanza kwenye uzinduzi wa Biblia ya Kisukuma.
Uzinduzi huo utafanyika katika kanisa la AIC Makongoro, Jumapili tar.27.6.2021 kuanzia saa 8 mchana hadi 12 jioni.
Muda huu utawapa nafasi waumini kutoka madhehebu mbali mbali kuweza kushiriki tukio hili, baada ya kumaliza ibada za Jumapili ndani ya makanisa yao.
Wanachama wote mnakaribishwa kushiriki tukio hili muhimu na la kihistoria kwa Chama cha Biblia, Kanisa na jamii nzima ya Kisukuma.
Upatapo taarifa hii mkaribishe na mwenzako, Wakristo kutoka madhehebu yote mnakaribishwa.
Tuunge mkono kwa kushiriki kikamilifu katika uzinduzi wa Biblia hii.
Tukutane AIC Makongoro kwenye uzinduzi wa Biblia ya Kisukuma Jumapili.
Karibuni 🙏🙏🙏
BIBLIA hiyo itakuwa inauzwa kwa bei ya punguzo.
Jiandae upate nakala yako pia.
Mungu ataongea na wewe kwa lugha yako ya Kisukuma.
Kazi ya kuamasisha makanisa na viongozi wa dini katika madhehebu mbali mbali ya Kikristo hapa nchini juu ya umuhimu wa kuwapatia watoto, vijana na wafungwa Neno la Mungu (Biblia), inaendelea katika Kanda ya kaskazini.
Na leo wajumbe wa Bodi wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Baba Askofu Amos Muhagachi na Mama Engineer Elikael Manase pamoja na Meneja wa Mahausino na Makanisa na Utunishaji mfuko wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Mch. Samweli Mshana wamemtembelea Mwl. Christopher Mwakasege ofisini kwake.
Tuzidi kuwaombea kwa kazi hii inayofanyika ili tujenge taifa lenye maadili mema.🙏
“MPATIE MTOTO, MFUNGWA NA KIJANA NENO LA MUNGU”
(ZABURI 119: 105; “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na Mwanga wa njia yangu.”)
Katika kipindi cha mwaka 2020 kupitia mpango wa Msamaria mwema Chama cha Biblia kiliweza kupata fedha kidogo kutoka UBS fedha iliyotuwezesha kutoa mafunzo ya UKIMWI kwa jamii kwa kushirikiana na makanisa, misikiti na wadau wengine walioko katika mapambano ya ugonjwa wa UKIMWI katika kata ya Hombolo, Ugogoni, Mmbande na Mpunguzi mkoani Dodoma.
Kutokana na ukosefu wa fedha ufadhili Chama hakikuweza kuendelea kutoa mafunzo katika maeneo mengine ambayo mpango huu ulikuwa unafanyakazi zake.
Kwa kushirikiana na makanisa, serikali za vijiji na wadau wengine katika kata zilizotajwa hapo juu, tuliweza kuwafikia watu 183 kwa mafunzo ( 85 wanaume na 98 wanawake) 285 vifaa kwa ajili ya kufundishia viligawiwa kwa washiriki kwa lengo la kuendeleza mafundisho na kuwafundisha wengine.
Watu 40 wenye ulemavu wa macho waliweza kufikiwa na mafunzo haya kutoka kata ya Ugogoni. Mafunzo haya yaliweza kuwapatia elimu ya jumla kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI na Virusi vya UKIMWI. Chama cha Biblia kimekuwa mdau wa kwanza kuwakutanisha na kuwapatia elimu hii ambayo hawajawahi kuipata mahali pengine popote. Kupitia mafunzo waliyoyapata imewasidia kujua jinsi ya kupambana na maambukizi ya UKIMWI baada ya kuonekana ni kundi lililo kwenye hatari kubwa, hawana uelewa juu ya UKIMWI, wananyanyapaliwa, na jamii inawachukulia kama watu wasio na thamani na ambao hawawezi kupata maambukizi kutokana na ulemavu walio nao.
Picha za Matukio katika Kata ya Ugogoni
Chama kinakabiliwa na changamoto ya fedha kuendesha mpango huu. Mafunzo haya yanahitajika sana kwenye jamii yetu ila kutokana na uhaba wa fedha umefanya mpango huu kutowafikia vijana walio wengi.
Wakagulu wapatao 756 wanawake wakiwa 550 na wanaume wakiwa 206 waliojiunga na mpango wa kujifunza kusoma na kuandika (LWA Kikagulu) mnamo tarehe 15/06/2020 hadi tarehe 30/11/2020 hatimaye walihitmu mafunzo hayo huku wakiwa na furaha kwa kujua kusoma na kuandika. Wakizungumzia furaha yao wameonekana wakiwa na bashasha na furaha sana kwa kupata elimu hii muhimu kwa maisha yao.
“Sasa ninaweza kusoma na kuandika na hata nikiumwa nikiandikiwa dawa sina haja ya mtu kunisomea na pia naweza kushiriki kikamilifu katika huduma za kijamii kama kupiga kura na mengine mengi katika dunia ya sasa” mama moja alisikika akisema maneno hayo kwa furaha.
Sherehe hizo zilifanyika tarehe 27/02/2021 katika Ukumbi wa Nazareth huko Gairo.
Mratibu wa mpango huu Mwl. Frank Makalla wa kwanza kushoto kwa waliokaa mbele akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu waliosimama nyuma wenye vyeti pamoja na mgeni rasmi Baba Askofu Paulo Jacob Mameo wa Kanisa KKKT Jimbo la Morogoro wa pili kutoka kushoto na wageni wengine walioalikwa kwenye mahafali hayo.
Baadhi ya wakinamama wenye umri mkubwa walioweza kushiriki na kupata vyeti vyao.
Kabla ya kugawa vyeti kulitanguliwa na hotuba na nasaa mbalimbali kutoka kwa Mgeni rasmi na viongozi mbalimbali walioalikwa kwenye mahafali haya ya tatu tangu kuanzishwa kwa mpango wa LWA Chikagulu katika mkoa wa Morogoro wilaya za Kilosa na Gairo
Canon Mstaafu Bonifas Mkami wa Kanisa Anglikani Jimbo la Morogoro
Canoni Mstaafu Bonifasi Mkami ni mmoja wa wachambuzi wa Biblia ya lugha ya Chikagulu inayoendelea kutafsiriwa katika lugha hiyo pia ni mmoja wa watu walioshiriki katika uandishi wa kitabu cha Chibweda. Akizungumza baada kupewa nafasi ya kuongoza ibada ya ufunguzi wa maafali alisema
“Mpango huu wa akina mama kujifunza kusoma na kuandika kwa lugha yao wenyewe kupitia Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama kikaona kianzie kwetu sisi wakagulu. Baada ya hapo tukaanza uandishi wa vitabu.
Kwanza cha Mwalimu, pili cha mwanafunzi kwa neema ya Mungu, mimi nilikuwa mmojawapo. Jina la Kitabu cha Mwanafunzi na Mwalimu tulikiita “CHIBWEDA” kwa maana ya FURAHA na kuweka picha zinazotoa taswira ya Kikagulu”.
Canon Mstaafu Bonifas Mkami wa Kanisa Anglikani Jimbo la Morogoro
Pia aliongeza kusema “Baada ya kukamilisha kuandika vitabu hivyo ikawa ni kazi ya kuwatafuta walimu wanaojua kuzungumza Kikagulu kwa ufasaha ili wapewe mafunzo ya kufundisha madarasa ya wanakisomo watakaojifunza kusoma na kuandika kwa kutumia lugha yao ya Kikagulu kwa kuwa ndiyo wanayoilewa Zaidi na baadae wanaweza kusoma na kuandika kwa Kiswahili na lugha zingine bila shida yoyote na baada ya hapo yakaanzishwa madarasa 10 ya kwanza na waalimu 20 katika awamu hii ya kwanza.”
Nasaha na shukrani za Canon Bonifasi Mkami
Kujua kwenu kusoma na Kuandika kutasaidia sana baada ya Biblia yetu sisi wakagulu tunayoiandaa kwa sasa na iko hatua za mwisho. Itakuwa rahisi ninyi kuisoma bila shida kwa hiyo tunatoa shukrani nyingi kwa Chama cha Biblia cha Finland na Chama cha Biblia cha Tanzania kuwezesha mpango huu katika mkoa wetu katika wilaya zetu za Kilosa na Gairo katika lugha hii ya Chikagulu Mwenyezi Mungu na awabariki sana.
Na zaidi tunawashukuru sana Mwalimu Frank Makalla mratibu wa mpango huu, Ndugu Timothy Kamau, Dr Suzan Nyaga na Ruth Munguth wa SIL Kenya.
Nawaombeni ninyi mliofaidika na mpango huu, muwe mawakili wema na waminifu katika kutunza lugha yetu.
Mratibu wa mpango huu wa LWA Chikagulu Mwalimu Frank Makalla
Akizungumza kabla ya kukabidhi vyeti kwa awamu ya tatu ya wahitimu hao, Mratibu wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Mwl.Frank Makalla alisema
“wahitimu hao ni wa awamu ya tatu ya programu hii iliyolenga kuwajengea uwezo wanawake kusoma na kuandika ambao kwa sababu mbalimbali hawakuweza kwenda shule wakati walipostahili kwenda shule, hii ni fursa kwao wakiwa watu wazima kuanzia aka 14 na kuendelea ingawa na wanaume wanaruhusiwa kushiriki japo si kwa kiwango kikubwa maana mpango unawalenga wanawake ambao hawakupata nafasi hiyo ya kusoma na kuandika kutokana na sababu mbali mbali.”
Mratibu wa mpango wa kusoma na kuandika wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Mwl.Frank Makalla akizungumza na wahitimu wa awamu ya tatu katika mahafali hayo huku akiwasisitiza wasiache kufanya yale waliyofundishwa pia wahakikishe kuwa kupitia wao watu wengi zaidi walijue Neno la Mungu.
Awamu ya kwanza waliohitimu ni jumla ya watu 97 ambapo wanawake ni 83 na wanaume ni 14 kutoka vijiji 10 vya Gairo na Kilosa ambavyo ni Gairo, Mtumbatu, Chakwale, Mamboya, Maguha, Berega, Mwandi,Magela, Mabula, pamoja na Italagwe.
Awamu ya pili waliohitimu jumla ni 248 ambapo wanawake ni 214 na wanaume ni 34; kutoka kwenye vijiji 10 vingine ambavyo ni Mogohigwa, Kibedya, Tabuhotel, Magubike, Nguyami, Ibindo, Ntembo, Mbili, Dumbaalume, pamoja na Kiegeya.
Waliojiandikisha ni 423 kati yao waliohitimu ni 317 na ambao hawajahitimu ni 106 kutokana na changamoto mbalimbali kama vile kuhama, shughuli za mashamba, na matatizo mbalimbali ya kijamii.
Aliendelea kusema kuwa mahafali hayo ni mwendelezo wa mahafali ya awamu ya kwanza ya program hiyo iliyoanza mwaka 2017, ambapo watu 120 walijiandikisha huku watu 97 walihitimu mafunzo hayo ambayo pamoja na kuwafundisha kwa kutumia lugha ya chikagulu kama lugha ya kufundishia kwa urahisi wa kuelewa kwa lugha yao lakini kadiri wanvyoendelea kujifunza kusoma na kuandika hatimaye wanaweza kusoma na kuandka katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine.
Alieza pia kuwa programu hiyo inafadhiliwa na Chama cha Biblia cha Finland na Chama cha Biblia cha Tanzania kikitoa usimamizi wa mpango na uratibu uku Summer Institute of linguistics (SIL) hawa wanatoa utaalamu wa waalimu pamoja na mwongozo wa kuandaa vitabu vya kufundishia. Programu hiyo inalenga zaidi kuwainua wanawake kujifunza kusoma na kuandika ingawa na wanaume wanakaribishwa kushiriki.
Wahitimu wa CHIBWEDA wakiwa katika kufuatilia hotuba na nasaha za viongozi wakati wa mahafali yao iliyofanyika mnamo tarehe 27/02/2021 huko Gairo siku ya Jumamosi.
Mratibu wa mpango huu Mwl. Makalla alisema kati ya watu wazima 395 waliohitimu, wanawake ni 337 na wanaume ni 58 katika awamu hii ya tatu
Aidha, Mwl. Makalla aliomba ushirikiano na serikali katika mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwafanya wananchi waliokosa fursa ya kusoma na kuandika kujiunga na kuendelea kupata elimu hiyo.
“Katika programu yetu hii tumekuwa tukichukua wale wenye umri wa kuanzia miaka 14 na kuendelea, hivyo wale wenye miaka 14 hadi 17, serikali inaweza kuwatambua na kuwaingiza katika mfumo wa MEMKWA katika shule za msingi kama ambavyo Serikali inaelekeza kupitia wizara ya Elimu ili wakajifunze zaidi kwa sababu sisi hapa tunawafundisha kusoma na kuandika tu huko watajifunza masomo mengine pia kama Hesabu, Sayansi, Jiografia Historia na kadhalika.
Changamoto ya kwa nini wanaanza wengi na kuhitimu wachache?
Sababu zilizotajwa ni kwamba jamii ya wakagulu ni wakulima na wafugaji kwa hiyo wakati wa masika wakulima wanahamia mbali na vijiji ambako ardhi ina rutuba zaidi kwa kilimo cheye kuleta tija, pili wafugaji wanahamia maeneo mengine kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao na matatizo mbalimbali ya kijamii.
Katibu wa UMAKI Ndg. Josephine Semwenda
Katibu wa idara ya maendeleo ya akina Mama UMAKI Josephine Semwenda katika Dayosisi ya Morogoro ambaye alialikwa kuwatia moyo wahitimu hao aliwasisitizia wahitimu kutokuogopa kuitangaza lugha ya Chikagulu kila mahali katika eneo lao la ukaguluni na kwingineko kwa kuwahimiza kuwa mabalozi wema katika kuilinda lugha yao isipotee, alitumia nafasi hiyo pia kuwapongeza. Wahitimu wote na kuwatakia kila lakheri katika kutekeleza majukumu ya kijamii na Kanisa.
Na hapa aliendelea kueleza zaidi kuwa
“Kwa Neema ya Mungu mmemaliza, Mungu aendelee kuwa karibu sana aendelee kuachia nguvu ya kuendelea kujifunza zaidi hata katika masomo mengine pia natamani kuona wengine hata mufike secondary kwasababu mmeshajua kusoma na baadae mtafika mbali Bwana Yesu asifiwe. Bila shaka kujua kusoma kwenu kutawasaidia sasa kuendeleza kusoma Neno la Mungu lakini pia kuweza kusoma vitabu mbalimbali na kufahamu mambo mengi ambayo usipojua kusoma na kuandika unakuwa kama kipofu na mambo mengi yanakupita.”
Sisi Idara ya UMAKI tunashukuru kwa ajili ya neema hii. Mana ninyi wahitimu mtakuwa nguzo muhimu kwenye madarasa yetu ya UMAKI kwa kuwafundisha na kuwaongoza wanawake kwenye madarasa yetu ya umaki na kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya idala ya kina mama ambao wengi wao hawajajua kusoma na kuandika. Maana wengine wanapoombwa kutoa Neno au labda kufundisha jambo fulani wengine huwa hawawezi kwa sababu hawajui kusoma na kuandika sasa wale wa madarasa ya umaki mtakuwa msaada mkubwa kwao.
Mwisho kabisa niendelee kupongeza tena na tena kwa juhudi ambazo mmezichukua hata kufikia siku ya leo Mungu awabariki lakini msiishie hapo muendelee kujiendeleza ili muweze kupata mambo makubwa zaidi na Jina la Bwana litaendelea kuhimidiwa kama sasa hivi unaweza kusoma masomo ya Biblia na muweze kusoma kwingine hata katika taifa letu pia Mungu awabariki muendelee kutimiza ahadi aliyo wapatia Bwana Yesu. Amina.
Diwani wa Kata ya Gairo na katibu wa Mbunge jimbo la Gairo Ndugu Danstan Mwegoha
Diwani Danstan Mwegoha aliwashukuru sana Chama cha Biblia cha Tanzania na wote waliotia mkono katika mpango huu kwa kutambua umuhimu wa wananchi wetu wakristo wetu kuendesha mafunzo ya elimu ya watu wazima na hasa kwa kuwalenga wakinamama ni msaada mkubwa kwao, sisi tunasema wakina mama ni jeshi kubwa kwa sababu wakina mama ndiyo wenye majukumu makubwa na akina mama ndiyo wenye malezi mazuri kwa watoto. Na pia wakina mama ndiyo wanaowatunza wakina baba.
Diwani Danstan Mwegoha akihutubia wahitmu
Na pia aliendelea kusema, Kwenye utaratibu wetu wa kutoa mikopo mara nyingi huwezi kukuta wakina baba wakiwa kwenye vikundi hivyo bali utakuta wakinamama, vijana, na walemavu, kwa hiyo wakinamama pamoja na vipato vyao vidogo wanaweza kuunganisha nguvu kwa kukopa na kulipa vizuri kuliko wakina baba.
Zamani ilikuwa ni vigumu sana kusomesha watoto wa kike kwa sababu wakina baba walikuwa wanahitaji kupokea mahali kwa kunufaika zaidi sasa bila kuangalia maisha ya binti zao kwa wakati ujao. Ninaishukuru sana serikali yetu inaonekana kuwajali na kuwalinda watoto wa kike katika kupata elimu.
Jukumu letu sisi kama serikali na Chama hiki kinacho endesha mafunzo haya tuombe sana kuwa na ushirikiano wa kutosha. Sisi kwa heshima yetu ya uongozi kwa mujibu wa nafasi yangu katika uongozi msisitizo na mkazo wa mtu kuchaguliwa na kupigiwa kura katika ngazi yoyote kuna vipengele vimeandikwa kwamba ni lazima mtu ajue kusoma na kuandika ndipo aruhusiwe kugombea nafasi na si vinginevyo kwahiyo unaweza kupata nafasi ya kuwa kiongozi kama diwani, mbunge, Rais n.k, kwa kuwa sasa mnajua kusoma na kuandika. Nawatakia Baraka za Mungu katika kuendelea mbele. Mungu awabariki sana.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nguyami.
Ndugu Mgeni rasmi, katika Kijiji changu sisi tumejiona fahari sana kwa kuwepo mpango huu na wengi waliohitimu katika mafunzo haya wamekuwa Baraka sana kwa kijiji chetu kwa maana miongoni mwao tulipata mama mmoja ambaye sasa ni mwekahazina anayeitwa Rehema Penford wa kijiji chetu. Kabla ya kupatiwa elimu hii haikuwa hivyo.
Na wananchi wengi wanawaamini watu wanaopitia elimu hii kwa kuwa wameonekana kuwa na ufahamu mkubwa na maadili mema katika Jamii yetu. Sisi kama serikali tunatafuta mpango mzuri wa kuwasaidia Chama cha Biblia cha Tanzania ili kiweze kuwafikia wengi zaidi katika Kijiji chetu.
Mwenyekiti wa Kijiji wa Kijiji cha Nguyami Mh. Gilbert Ngiga
Ushauri wangu kwenu wahitimu wa CHIBWEDA nawaomba sana, huu uwe mwanzo wa kutaka kujiendeleza zaidi na zaidi ili mfikie ndoto zenu. Na nyinyi pia ni rahisi serikali kuwasaidia mikopo katika kujiendeleza kwenu kwa maana kumuelimisha mwanamke umeielimisha jamii yote.
Zaidi nawapongeza tena Chama cha Biblia kwa kuwezesha mpango huu na mimi naahidi kujiunga na Chama hiki ili nami nitoe mchango wangu hata kwa pesa kidogo na Mwenyezi Mungu na awabariki sana.
Meneja wa miradi na utunishaji wa mfuko wa CBT Mchungaji Samwel Mshana.
Mch. Samweli Mshana ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania alisema
Mgeni rasmi, Baba Askofu Paulo Jacob Momeo, Mheshimiwa mratibu wa UMAKI, Mheshimiwa mratibu wa mpango, Mheshimiwa Canon mstahafu, mheshimiwa Mwenyekiti wa kijiji cha Nguyami, waandishi wa habari, mheshimiwa mratibu wa Chibweda, walimu na wahitimu wote, Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe.
Kwanza, nianze kumshukuru Baba Askofu lakini pili nimshukuru sana mheshimiwa Diwani kwasababu kweli mara ya kwanza lakini kwa sababu mimi ni Meneja wa miradi hii ni mara ya kwanza kuwa na viongozi wa serikali. Mheshimiwa Diwani tunakushukuru karibu sana lakini sitaacha kushukuru pia mwenyekiti wa kijiji cha Nguyami umetoa ushuhuda chanya unao onyesha faida ya mradi huu wa CHIBWEDA na pia tuwashukuru waalimu kwa jinsi ambavyo mmekuwa mkijitoa kwa jinsi ambavyo mme onyesha juhudi sio jambo rahisi kwa kiufupi umfundisha mwanafunzi mpaka afikie hatua ya kusoma na kuandika kama ambo tumeshuhudia mama yule alivyo soma risala Mungu awabariki sana.
Mchungaji Mshana akiongea na wahitimu wa awamu ya tatu wa Chibweda wakati mahafali hayo huko Gairo.
Wahitimu wa leo kwa niaba ya Katibu Mkuu napenda kuwapongeza.
Najua kwamba mmevumilia mambo mengi wakati wakusoma wengine mlipata changamoto za hapa na pale lakini kwa neema ya MUNGU mmeweza kuvumilia yote hayo na mmefika hatua ya mwisho.
Mimi nasema hongeleni sana na Chama cha Biblia kinaona fahari sana kwaajili yenu, mme tufanya kumtukuza Mungu kila tunapo waona hasa katika juhudi zenu na jinsi ambavyo mmefikia hatua hiyo kwakweli sisi mmejawa furaha na mmetufanya tumtukuze MUNGU kwaajili yenu na mimi kama Meneja wa miradi na muakilishi wa Katibu Mkuu sito acha kusema elimu na bidii kama ambavyo mmesikia viongozi wanavyo sema ukisoma
Wakolosai 1 : 10 “mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu;
Kwahiyo matunda ya elimu hiyo muyafanye na baadhi yenu kule kijijini hata ajira za vijiji sasa mnaachiwa maana mwazoni ilikuwa sio rahisi, na kwa sababu ya elimu muliyo ipata imewasaidia sana na sasa mnaweza kuajirika.
Mgeni rasmi Baba Askofu Paulo Jacob Mameo
Mgeni rasmi kabla ya kutoa vyeti kwa kundi la tatu la wahitimu wa Chibweda ‘Furaha’ Baba Askofu Momeo wa KKKT aliwataka wahitimu hao kutumia maarifa hayo kujiendeleza kiuchumi na kushiriki katika uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mgeni rasmi; Baba Askofu Paulo Jacob Mameo akiwa anazungumza na wahitimu wa awamu ya tatu katika mahafali hayo katika ukumbi wa Nazareth Gairo.
Baba Askofu Memo aliendelea kuwatia moyo na kuwahimiza kuendeleza kuenzi lugha yao ya Kikagulu na uku wakitumia maarifa hayo waliyoyapata kusaidia kueneza injili kwa watu wengine kwa maana sasa wanaweza kusoma na kuandika na kuwasaidia wengine uko vijijini wasiojua bado kusoma Biblia.
Mwisho nichukue nafasi hii kwa niaba yangu na Kanisa kuwashukuruni Chama cha Biblia cha Tanzania kwa jitihada nzuri ya kufuta ujinga kwa kusoma na kuandika kwa kuanzisha elimu ya watu wazima hasa kupitia kusoma Biblia. Mradi huu ni kitu kizuri sana sio tu kwa kufuta ujinga bali pia kwa kueneza maandiko matakatifu ya Neno la Mungu, Mungu aendelee kuwabariki ili habari njema iendelee kuenea kwa mbinu kama hii ya kufuta ujinga wa kutokusoma na kuandika. Mungu aendelee kuwapa maono zaidi ili huduma hii iendelee. Amina!
Katika mahali hayo burudani ilikuwa sehemu ya sherehe hizo, ambapo wahitimu hao pamoja na walimu wao walionesha michezo na nyimbo mbali mbali za kusifu na kushukuru wadau mbali mbali waliofanikisha wao kupata elimu hii.
Na hapa ni vikundi mbalimbali vya wahitimu wakitoa shukurani zao kupitia njia mbalimbali zikiwemo vile nyimbo, ngonjera pamoja na usomaji wa risala mbele ya mgeni rasmi.
Wahitimu wa awamu ya tatu ‘CHIBWEDA’ wakiimba wimbo maalumu wa kukishukuru Chama cha Biblia cha Finland na Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kuwaletea mpango huu wa kujifunza kusoma na kuandika.Pichani, ni wahitimu wa awamu ya tatu Chibweda, wakisoma Risala mbele ya mgeni rasmi wakati wa sherehe hiyo.