WAKATI Chama cha Biblia cha Tanzania kikiwa kimetoa msaada wa Biblia Takatifu kwa wafungwa na mahabusu ya Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko yote ya jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Gereza la Segerea, SSP. Daniel Mwakyoma amesema ukosefu wa uzio na upungufu wa nyumba za watumishi ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili gereza hilo.
Makabidhiano ya msaada huo upande wa Gereza la Segerea yamefanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Arch. Ng’wilabuzu Ludigija na Maafisa Waandamizi wa gereza hilo, huku upande wa Chama cha Biblia kikiwakilishwa na wajumbe mbalimbali akiwemo Katibu wa Chama hicho, Mch. Alfred Kimonge, Meneja wa Mahusiano ya Makanisa na Utunishaji wa mfuko wa chama hicho, Mch.Samwel Mshana huku Kanisa Katoliki likiwakilishwa na Mjumbe wa Bodi wa Chama hicho hicho, Padri Chesco Msaga, CPP.S ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo ulioenda sambamba na utoaji wa mahitaji ya kimwili kwa wafungwa na mahabusu hao, unaojumuisha sabauni na dawa ya meno, Katibu wa Chama hicho, Mch. Kimonge amesema, lengo ni kuwapa wahusika fursa ya kusoma Neno la Mungu, linalobadilisha, na kutia faraja, msaada uliopokelewa kwa furaha na wahusika.
“Chama cha Biblia Tanzania ambacho kinajumuisha wanachama kutoka madehebu ya Waprotestanti, Wasabato, Wapentekoste na Wakatoliki, kinaguswa na maisha ya makundi mbalimbali wakiwemo mahabusu na wafungwa kama nyie, hivyo Biblia hizi tunazokabidhi kwenu tunaomba ziwasaidie kufanyie rejea yale mnayohubiriwa…zinafaa hata kwa wale wasiokuwa Wakristo,” amesisitiza.
Msaada huo umeenda sambamba na ziara maalum ya Mkuu mpya wa Wilaya ya Ilala, Arch, Ng’wilabuzu Ludigija kutembela magereza yaliyopo wilayani kwake ya Segerea na Ukonga, kama sehehemu ya kujitambulisha.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Wilaya na wajumbe wa Chama cha Biblia, walipata fursa na kuzungumza na uongozi wa gereza hilo pamoja na kukutana na mahabusu na wafungwa, wakiwemo wanawake na wanaume ambapo waliwasilisha changamoto zao.
Upande wake SSP Mwakoyoma amesema ngome (gereza), haijazungushiwa uzio, hali inayosababisha hali ya usalama kuwa hatarini, hali inayoenda sambamba na ukosefu wa nyumba za watumishi kiasi cha kusababisha asilimi 90 kuishi uraiani nje ya kituo chao cha kazi.
Changamoto nyingine kama zilivyobainishwa na Mkuu huyo wa Gereza ni ukosefu wa huduma ya usafiri kwa mahabusu pindi wanapotakiwa kupelekwa mahakamani kusikiliza kesi zao, uhaba wa maji na kutokuwa na jenereta (standby generator) pindi umeme unapokatika, jambo ambalo ni hatari kwa jumuiya yenye msongamano wa watu kwani pia kuna mlundikano wa mahabusu.
Akitoa kero zinazowakabili wafungwa na mahabusu wanawake, nyampala wa kundi hilo, (jina tunalihifadhi) amesema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni baadhi ya watuhumiwa kuchanganyikiwa kiakili, hali inayosababishwa na masuala mbalimbali likiwemo la kesi zao kutokusikilizwa kwa wakati, jambo ambalo amesema ni hatari kwa wafungwa na mahabusu wengine.
“Kuathirika kisaikolojia… anapiga mahabusu wenzake na anaweza hata kuwafanyia vitendo vingine vya kikatili zaidi, hivyo tunaomba hili liangaliwe na kufikishwa kunakostahili ili ikiwezekana hata wafanyiwe vipimo vya kitaalam zaidi na ikibainika ni shida, basi wapelekwe kwenye magereza yaliyotengwa kwa watu wa namna hii,” amesema.
Changamoto nyingine kwa wanawake ni uhaba wa magodoro hali inayowalazimu baadhi yao kulala chini kwenye sakafu, uhaba wa sare kwa wale ambao tayari wameshahukumiwa, lishe duni kwa watoto wanaoishi na mama zao gerezani pamoja na uhaba wa maji na vifaa vya usafi vya kutosha hali inayosababisha wengi kupata ugonjwa wa UTI.
Asia Mhamed ambaye ni mahabusu Na.125/2016 yeye amesema changamoto zaidi ipo kwa watuhumiwa wa kesi za mauaji, utakatishaji pesa na dawa za kulevya, ambapo amedai zimekuwa hazikilizwi kwa kile wanachoambiwa na mahakimu na majaji wanaosikiliza kesi hizo kuwa wanaendelea na upepelezi na hata wakati mwingine kudai kwamba kesi hizo uendeshaji wake unahitaji hela ambayo lazima iwe imetengwa kwenye bajeti ya serikali.
Upande wa mahabusu na wafungwa wanaume, mwakilishi wa kundi hilo, Florian Apolynal yeye amesema licha ya baadhi ya watuhumiwa wakiwemo wale wanaokabiliwa na kesi za Uhujumu Uchumi kutekeleza agizo la Rais, la kuandika barua na kutaka kufanyike maelewano (bargaining), lakini hawajui kinachoendelea baada ya kutekeleza hilo.
Pia wamedai kuwa kuna changamoto ya kubambikiziwa kesi zikiwemo za mauaji “… wakishakukamata wanakupa adhabu kali zenye mateso ili wakubadilishia kosa ambalo haujafanya… hivyo wengi humu tuna machungu kwani unakamatwa na kosa la wizi (robbery), lakini kwenye faili unaandikiwa mauji,” amesema mahabusu Charles Raphael Mkanya.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kero hizo amezipelekea na atazifikisha ofisini kwake ajadiliane na wataalam na kile kitakachoshindikana atakipeleka ngazi za juu zaidi ili zipatiwe ufumbuzi.
Watu wazima 317 kati ya 423 kutoka vijiji 20 wameitimu mafunzo ya kusoma na kuandika kwa lugha ya Chikagulu.
Akizungumza jana baada ya kukabidhi vyeti 89 kwa awamu ya kwanza ya wahitimu hao, Mratibu wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Frank Makalla alisema wahitimu hao ni wa awamu ya pili ya programu iliyolenga kuwajenga uwezo wa kusoma na kuandika watu wazima wanaoanzia miaka 15 na kuendelea.
Mratibu wa Mradi Mwl. Frank Makalla
Mratibu wa mpango wa elimu kwa watu wazima kutoka Chama Cha Biblia Cha Tanzania akiongea jambo katika mahafali ya awamu ya pili iliyofanyika GairoAwamu ya kwanza ya programu hiyo iliyoanza mwaka 2017, watu 120 walijiandikisha huku watu 97 walihitimu mafunzo hayo ambayo pamoja na kuwafundisha kwa lugha ya Chikagulu, mafunzo hayo yanafanywa pia kuweza kusoma na kuandika kwa Kiswahili.
Programu hiyo inafadhiliwa na Chama cha Biblia cha Tanzania, Chama cha Biblia cha Finland na Taasisi ya Lugha ya Kenya, pia unalenga zaidi kuwainua wanawake ingawa na wanaume wanaruhusiwa kushiriki.
Makallla alisema kati ya watu wazima 317 waliohitimu, wanawake ni 270 na wanaume ni 47.
Akizungumzia sababu ya baadhi ya watu waliojiandikisha kushindwa kumaliza, Makallla alisema kwa wale walioacha masomo, hao wamepewe nafasi ya kuingia darasa la awamu ya tatu linalotarajia kuanzia Mei 15, mwaka huu ikiwa ni baada ya walimu kupewa mafunzo ya kujengewa uwezo.
Aidha, Makalla aliomba ushirikiano na serikali katika mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwafanya wananchi waliokosa fursa ya kusoma na kuandika.
“Katika programu yetu tumekuwa tunachukua wale wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea, hivyo wale wenye miaka 15 hadi 17, serikali inaweza kuwatambua na kuwaingiza katika mfumo wa MEMKWA ili wakajifunze Zaidi kwa sababu sisi hapa tunawafundisha kusoma na kuandika tu, ” alieleza.
Mgeni rasmi Dk. Jackson Nyanda (Makamu Mwenyekiti Chama cha Biblia cha Tanzania)
Kabla ya kutoa vyeti kwa kundi la kwanza la wahitimu wa 89 wa Chibweda ‘Furaha’ Dk Jackson Nyanda aliwataka wahitimu hao kutumia maarifa hayo kujiendeleza kiuchumi na kushiriki katika uchumi wa taifa kwa ujumla.
Meneja Miradi na Uhusiano wa Makanisa Mch. Samwueli Mshana
Naye Meneja wa Miradi na utunishaji mfuko wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Samwueli Mshana ambaye pia alimwakilisha Katibu wa chama hicho, alisema lengo la chama chake ni kutafsiri Biblia kwa lugha za asili, kukuza na kutunza lugha ya asili lakini pia kusaidia jamii husika kuelewa Neno la Mungu.
Na. Ndugu Frank Makalla (Msimamizi Mkuu wa Mradi-CBT).
Chama Cha Biblia Cha Tanzania kilianzisha kisomo cha elimu ya watu wazima kwa kushirikiana na Chama Cha Biblia Cha Finland na SIL (Summer Institute of linguistic) mnamo mwaka 2017 na mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa kuandaa vitabu kwa ajili ya wanakisomo wa elimu ya watu wazima katika msemo wa Kikagulu na kanisa katika eneo hilo lilishiriki kikamilifu kwa kutoa watafsiri na waandishi. Ndipo mradi ukaanza 2018 ukiwa na walimu 20 (ishirini). Walimu hao walianza na wanafunzi mia ishirini ambavyo wanafunzi 97 walihitimu na kupewa vyeti mwezi machi 2019.
Na baada ya hapo Madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika yalianza mwezi wa nane 2019 katika vijiji 20 (ishirini) vingine na kila kijiji kina darasa moja na kila darasa lina walimu wawili 2 (wawili) na jumla ya wanafunzi ni 423 kwa vijiji vyote.
Madarasa hayo ishirini yanaendelea vizuri katika kiwango cha 97% (asilimia tisini na saba) wanaweza kusoma na kuandika. Tunatarajia watahitimu mwisho wa mwezi huu wa February 2020 na mahafali yatakuwa mwezi wa tatu kuanzia tarehe 14/03/2020 (kumi na nne), 21/03/2020 (ishirini na moja) na 28/03/2020 (ishirini na nane) kwa maana yamegawanywa kwenye vituo vitatu ambavyo ni Gairo, Nguyami na Magubike.
Darasa la Chibweda kijiji cha Kibedya
Mwalimu Devotha Madihi wa darasa la Chibweda kijiji cha Kibedya akifundisha darasani. Darasa hili lina mama mmoja mwenye watoto mapacha wanaonekana hapo chini na amekuwa akihudhulia vizuri sana darasani.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Berega
Wanakisomo wa darasa la Kikagulu katika Kijiji cha Berega wanajifunza kusoma na kuandika kwa kutumia lugha ya Kikaguru wakifundishwa na waalimu wao Rose Chitemo mwenye kilemba na Sofia Muhumba.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Berega
Mwanafunzi Merina Malali wa Darasa la Chibweda Berega akiwa anaandika kufuatia maelekezo ya waalimu.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Kiegea
Darasa la Kiegea wanafatilia mafundisho ya mwalimu ubaoni.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Tabuhoteri
Darasa la kijiji cha Tabuhoteli lina wakina mama wenye umri mkubwa na wana bidii sana katika kujifunza kusoma na kuandika.
Darasa la Chibweda Kijiji cha Ibindo
Wanakisomo katika kijiji cha Ibindo wakipata maelekezo kutoka kwa walimu wao kuhusu kusoma na kuandika.
Kujifunza kuandika
Mwanafunzi Merina Malali wa Darasa la Chibweda (mwenye kilemba cha pink) katika kijiji cha Berega akiwa anaandika kufuatia maelekezo ya waalimu.
Wanakisomo awa, wapo katika marudio wakisubiri kupewa mitihani yao ya mwisho ili hatimaye kukabidhiwa vyeti kwa wale watakaofaulu na kuhitimu masomo yao vizuri.
CHANGAMOTO:
Kwa kuwa hawa ni watu wazima zipo changamoto mbali mbali zinazoathiri mahudhurio darasani kama vile:- kazi za shamba, misiba kijijini na nje ya kijiji, kuumwa, kuuguliwa, mito kujaa na kuwatenganisha kwa muda, kutomaliza silabasi yao kwa wakati kwa kuwa wapo wenye kujifunza kwa polepole kulingana na umri wao na kusababisha waalimu kuwa fuatilia na kuwaelekeza kwa muda zaidi. n.k.
Changamoto katika kuwafikia
Wakati mwingine kuna changamoto ya kuwafikia wanakisomo kwa sababu ya ubovu wa miundombinu hasa barabara kama picha inavyoonesha hapa chini.
Kunasua gari
Wakati mwingine kipindi cha mvua changamoto kubwa ni barabara, mfano picha hiyo hapo Gari lilikwama kwenye matope kutokana ubovu wa barabara wakati tunakwenda kuona darasa la Mtumbatu na tulisaidiwa na wanakijiji kulinasua gari kwenye matope (Ndugu Frank Makalla akieleza).
Kutokana na kikao cha mapitio ya maendeleo ya mradi wa tafsiri ya Biblia kwa Lugha ya Kirimi November 04-09, 2019, Mkoani Singida, Tafsri bingwa Dr.Samy Tioye kutoka UBS athibitisha mradi huu kuendelea vizuri na umefikia hatua nzuri zaidi kwa hali hiyo Biblia ya Lugha ya Kirimi tunaitegemea iwe imekamilika 2020 December.
Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kushirikiana na Kanisa tunafanya kazi ya kutafsiri Biblia kwa Lugha ya Kirimi. Kazi hii inafanyika kwa ustadi mkubwa na kuzingatia kanuni na utalaam wa tafsiri ya Biblia kutoka muungano wa vyama vya Biblia Ulimwenguni (UBS).
Kwa mantiki hiyo hapa chini katika picha tunaona Dr.Samy Tioye mmoja wa watafsiri Bingwa wa Lugha kutoka UBS akiwa na watafsiri wa Lugha ya Kirimi katika kuangalia usahihi wa kazi hii muhimu.
Kirimi team, Singida, Tanzania
Mshauri bingwa wa Tafsiri za Biblia Dr.Samy Tioye akiwa anawaonyesha aina mbalimbali za tafsiri za Biblia na namna zinavyoweza kutumika kusaidia tafsiri ya Biblia kwa Lugha ya Kirimi, Katika ofisi ya tafsiri ya Biblia kwa Lugha Kirimi Mkoani Singida.
Maelekezo
Mshauri bingwa wa Tafsiri za Biblia Dr.Samy Tioye akiwa anaelezea jambo kwa watafsiri wa Biblia kwa Lugha ya Kirimi, Katika ofisi ya tafsiri ya Biblia kwa Lugha Kirimi Mkoani Singida.
Umakini
Watafsiri wa Biblia kwa Lugha ya Kirimi (Mch. Elia Mande na Mch. Simoni Kusina) wakipitia na kufanya masahihisho ya kitabu cha Kumbukumbu la torati.
kusaiisha
Mrs. Joyce Shisha, Katibu muhutasi wa mradi wa Kirimi akiingiza masahihisho ya kitabu cha Kumbukumbu ya tarati kwenye Programu maalumu ya Tafsiri za Biblia iitwayo Paratext.
Pamoja
Picha ya pamoja kati ya Meneja wa Tafsiri, mtafsiri Bingwa pamoja na watafsiri wa Biblia kwa Lugha ya Kirimi.