by The Bible Society of Tanzania | Jul 10, 2019 | Fundraisers, News, Refugees
CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA
N0: 01 July 2019, NEWSLETTERS /BARUA YA UPENDO YA KILA MWEZI
16 Hatibu / 9th Road, Madukani Area, P.O Box 175, Dodoma Tanzania. || T: +255 (026)-2324661 F: +255 (026)-2324058 || Email: info@biblesociety-tanzania.org || Site: www.biblesociety-tanzania.org
KWA WANACHAMA WA CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA NA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA.
Umoja wetu katika Kristo!
“Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”. (Yohana 17:21-23).
Umoja wa Kanisa ndiyo ishara ya mwili wa Kristo katika Ulimwengu. Kanisa ni familia ya Mungu katika ulimwengu huu, ni jumuiya ya watu wa Mungu wamwaminio Yesu Kristo katika maisha yao wakimsifu na kumshangilia Mungu katika ushuhuda na kuwaleta wengine ili wamjue Mungu wa kweli katika maisha yao. Chama cha Biblia cha Tanzania kimeendelea kwa uaminifu wote kulihudumia kanisa la nchi yetu kwa umoja wake kwa kuwapatia Maandiko Matakatifu [Biblia] ili kuliwezesha kanisa kuwa na Biblia katika mifumo na tafsiri mbali mbali kwa ajili ya uinjilisti na utume wake.
Kwa unyenyekevu mkuu nawaalika Wakristo wa madhehebu yote katika nchi yetu kushiriki katika huduma hii.Nakuomba ukiombee na kukichangia Chama cha Biblia cha Tanzania ili kipate fedha kwa ajili ya kutafiti, kuchapisha na kusambaza neno la Mungu kwa watu wote. Ni maombi yangu kwamba asiwepo Mtanzania hata mmoja anayetamani kulisoma neno la Mungu akalikosa kwa sababu ya gharama kubwa. Mwaka huu tuna lengo la kuwapatia watoto, vijana na wafungwa Biblia. Kwa ushirikiano wa kanisa la Mungu hapa nchini, tunaweza kuwafikia watoto, vijana na wafungwa ili kujenga Taifa la wacha Mungu. Kwa sadaka yako na matoleo yako ya upendo utakuwa baraka kwa kumpatia mtoto, kijana na mfungwa kule gerezani neno la uzima.
Nakutumia barua hii ya upendo kukualika na kukukaribisha ili ushiriki pamoja nasi kulijenga Taifa letu kiroho ili liwe taifa lenye kumhofu na kumcha Mungu. Ombea Taifa letu ili watu wake walipende na kulisoma Neno la Mungu.
Ni kiu yangu kwamba kila mtoto, kijana na mfungwa awe na Biblia yake mkononi.
Neema na Amani ya Kristo iwe pamoja nawe.
Alfred E. Kimonge
Katibu Mkuu
HAMASA YA KUFUNGUA MATAWI MIKOANI

Hawa ni Wanachama wa Tawi la Kitivo cha Sayansi ya Jamii moja ya matawi matatu katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Tunamshukuru Mungu kwa kuanza mwaka huu kwa baraka zake na uamsho mpya wa Makanisa na Wakristo kujiunga kwa wingi kuwa wanachama wa Chama cha Biblia cha Tanzania. Hadi sasa tumefanikiwa kufungua matawi kama ifuatavyo;
1. Dodoma – Chuo Kikuu cha Dodoma [UDOM ]
i. Tawi la Kitivo cha Elimu – Wanachama 120
ii. Tawi la Kitivo cha Biashara na Utawala – Wanachama 78
iii. Tawi la Kitivo cha Sayansi ya Elimu ya Jamii – Wanachama 110
2. EAGT Buhemba Tarime – Wanachama 210
4. Umoja wa makanisa – Kilimanjaro
5. Marangu-Kilimanjaro
6. Umoja wa makanisa – jiji la Mwanza
Na bado hamasa inaendelea katika maeneo mengine likiwamo jiji la Dar es Salaam na Tabora.

Viongozi wa Makanisa ya Moshi ambao ni waanzilishi wa Tawi la Chama katika Mkoa wa Kilimanjaro

Mwenyekiti wa Tawi la EAGT Buhemba Tarime akimkabidhi mchango wake Askofu Muhagachi Balozi wa Chama cha Biblia cha Tanzania.
Tunakuomba ushiriki katika huduma hii kwa maombi yako,unaweza kuchangia kila mwezi Tsh 2000,______ Tsh 5000,______Tsh 10,000,_______au kuchangia kwa mwaka Tsh 25,000, ____Tsh 50,000,_____Tsh 100,000 au zaidi. Kwa sadaka yako ya upendo unaweza kumfanya/kumgusa mtoto, kijana na mfungwa kumjua na kumfuata Kristo.
Nakualika kushiriki pamoja na Wakristo wengine waaminifu kwa kuchangia na kutuma mchango wako kwa akaunti ya M-PESA ya Chama cha Biblia cha Tanzania namba 890890 kisha tuma ujumbe wa kuchangia katika namba hizi: 0762998819, 0754383636 na 0754479789.
Pia unaweza kuchangia kupitia akaunti za Benki za DTB na NBC zilizoonyeshwa hapa chini.
Kwa DTB Akaunti Namba: 0901969001; SWIFT OR WIRING CODE DTKETZTZ
Kwa NBC Akaunti Namba: 029103000362

Akaunti Namba: 0901969001; SWIFT OR WIRING CODE DTKETZTZ

Akaunti Namba: 029103000362
Mungu na akubariki.
Askofu Amos Muhagachi
Mhariri.
Mawasiliano yatumwe kwa: Katibu Mkuu Chama cha Biblia cha Tanzania, P.0. Box 175, Dodoma, Tanzania. Email: aekimonge@yahoo.com T: +255262324661 Mob: +255754383636
by The Bible Society of Tanzania | Dec 3, 2018 | Appeal, Fundraisers, News
CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA

KUWEZESHA UPATIKANAJI WA MAANDIKO MATAKATIFU KATIKA LUGHA INAYOELEWEKA VIZURI NA KWA BEI WANAYOIMUDU
1.Chama cha Biblia cha Tanzania ni nini?
Chama cha Biblia cha Tanzania ni Shirika la Kikristo lisilo la Kidhehebu lililoandikishwa mwaka 1965 chini ya Sheria ya Udhamini wa Vyama.
Chama cha Biblia cha Tanzania ni Mshiriki wa Muungano wa Vyama vya Biblia ulimwenguni ( United Bible Societies –UBS ) ambao kazi yake kubwa ni uenezaji wa Neno la Mungu kwa wingi na uhakika kama ifuatavyo:
– Kueneza Neno la Mungu katika Lugha na Mawasiliano yanayokidhi mahitaji ya watu wengi Ulimwenguni.
– Kueneza Neno la Mungu katika Tafsiri sahihi bila kupoteza uhalisi wa Maandiko Matakatifu.
– Kuyauza Maandiko kwa bei wanayoimudi ili waweze kulifahamu Neno la Mungu.
- Kaziya Chama cha Biblia ilianza lini Tanzania?
( i ) Wamisionari wa kwanza kabisa nchini Tanganyika ndio walioanzisha kazi ya Chama kwenye karne ya 19.
( ii ) Kazi ya kueneza Biblia iliendelea kukua na mwaka 1982 Chama kilifikia ngazi ya kuwa Mshiriki wa Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni na mwaka 1988 Chama kilipata uanachama kamili wa Muunganohuu.
3.Je kazi za Chama cha Biblia cha Tanzania ni zipi?
Chama cha Biblia cha Tanzania ni chombo cha Kanisa kinachotumika katika kutekeleza utume wa Kanisa wa kuihubiri Injili kwa kila mtu. Chama cha Biblia kinafanya yafuatayo:
a ) Kutafsiri Biblia katika Lugha mbalimbali za kienyeji.
b ) Kuchapisha katika Mitindo mbalimbali:
– Biblia nzima.
– Maagano na
– Sehemu zake kwa wasomaji wapya.
c )Kueneza Biblia,Maagano na sehemu zake kwa watu wote kwa kushirikiana na :
– Makanisa na Mashirika yake.
– Maduka ya Vitabu.
– Watu binafsi pamoja na wakereketwa wa kujitolea.
d )Kushirikiana na Vyama vingine katika kuhakikisha Biblia inasomwa kwa lugha zote za hapa Tanzania ili kila mtu auonje uzuri wa Yesu Kristo na kupata maisha mapya.
- Je, hadi sasa Chama cha Biblia cha Tanzania kimetafsiri Biblia katika Lugha zipi za kienyeji ?
Chama hadi sasa kimemudu kutafsiri Biblia nzima katika Lugha za: Kiiraqw, Kihaya, Kinyakyusa, Kisukuma, Kijaluo, Kimasai na Kigogo. Pia kimeweza kutafsiri Agano Jipya katika Lugha za Kibena, Kimashami, Kivunjo, Kimochi, Kichasu( Kipare ), Kijita, Kidatooga, Igikuria, Kishambala, Kizaramo, Kinyiramba na Kirimi ( Kinyaturu ) Miradi ya Tafsiri inayoendelea ni ya Lugha za Kihehe, Kikaguru, Kiha na Kisukuma cha kisasa. Mbali na kuchapisha Biblia, pia Chama kinachapisha matoleo yafuatayo:
– Sehemu za Biblia.
– Sehemu za Biblia kwa wasomaji wapya wanaojifunza Biblia kwa Kiingereza, Kiswahili na Lugha za Kienyeji.
– Vipeperushi maalum vya vifungu vya Biblia kwa matukio mbalimbali k.m kuzaliwa kwa Yesu,kifo cha Yesu,wagonjwa waliolazwa,na matukio mbalimbali k.m Uhuru, Rushwa nk.
– Kanda naswa za Neno la Mungu.
– Neno la Mungu katika Braille kwa wasomaji wasioona.
– Neno la Mungu kwa maandishi makubwa kwa wenye udhaifu wa macho.
Kwa kawaida tafsiri inafanywa kutoka katika Lugha za asili za Kiyunani na Kiebrania,na hivyo kazi ya Tafsiri ni ngumu, inahitaji uangalifu wa hali ya juu na
inachukua miaka kati ya 8 hadi 10 kutoa toleo moja, kama kuna watafsiri walioajiriwa kwenye mradi kwa wakati wote na kuna wachambuzi 10-15.
- Je Chama cha Biblia kinapata wapi fedha za kukiendesha?
Chama cha Biblia cha Tanzania kinaendeshwa kwa michango ya
– Makanisa.
– Taasisi mbalimbali za Makanisa.
– Watu binafsi ambao ni wanachama.
– Marafiki wa Chama.
– Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni ambao unatoa misaada ya Maandiko Matakatifu kutoka nje ambayo Chama kinayauza na kutumia sehemu ya mapato kuendesha huduma.
- Je Chama cha Biblia cha Tanzania kina mahitaji gani?
Ili kutekeleza kazi zake za Kutafsiri, Kuchapisha na Kueneza Maandiko Matakatifu Chama cha Biblia chaTanzania kinahitaji kiasi kisichopungua Dola Milioni moja za Marekani kwa mwaka. Kama Kanisa na Wakristo binafsi watakuwa wanachangia kila mwaka kwa uaminifu Chama kinaweza kuendesha kazi zake vizuri.
- Je, unawezaje kusaidia kazi za Chama cha Biblia ?
Kuna njia nyingi za kukisaidia Chama cha Biblia katika kazi zake na kinamualika kila Mkristo kushiriki yafuatayo:-
( i )Kujiunga na kuwa Mwanachama na kuchangia
– Uanachama wa Maisha Mme na Mke shilingi 15,000= na ahadi isiyopungua shilingi 15,000=kwa mwaka.
– Uanachama wa Maisha mtu mmoja shilingi 10,000= na ahadi isiyopungua shilingi 10,000= kwa mwaka.
– Uanachama wa kawaida (bidii ) shilingi 5,000=kwa mwaka.
– Uanachama wa kawaida kwa Wanafunzi wa Sekondari na Vyuo shilingi 2,000= au zaidi kwa mwaka.
– Uanachama wa kawaida wa kushirikishwa kwa watoto na wanafunzi wa shule za Msingi shilingi 1,000= au zaidi kwa mwaka.
– Uanachama wa Mashirika shilingi 50,000= na mchango usiopungua shilingi 50,000= kwa mwaka.
– Mwanachama wa Biblia Moja kwa Mwezi ( Bible a Month Club) 5,000=, 10,000=, 15,000=, 20,000= au zaidi kwa mwezi.
(ii )Tafsiri.
Unaweza kusaidia Chama kwa :
– Kuchangia Miradi ya Tafsiri kwa kutoa fedha taslimu.
– Kuchangia Miradi ya Tafsiri kwa kuwapata Watafsiri wenye uwezo na Wachambuzi wenye mzigo na kazi hii.
– Kuchangia Miradi ya Tafsiri kwa kupitia Miswada ya Tafsiri.
(iii ) Uhamasishaji.
-Kutoa sadaka au michango kila mara kwa Chama.
– Kuhamasisha Makanisani juu ya Wiki ya Biblia ambayo ni kila wiki ya kwanza ya Mwezi Novemba kila mwaka.
– Kuanzisha Vikundi vya Biblia Moja kwa Mwezi ( Bible a Month Club-BAMC ) kwenye Makanisa na maeneo ya kazi.
– Kusaidia kueneza Biblia kwa njia ya kuuza kwa kujitolea.
– Kutoa njia mbadala au mawazo ya jinsi ya kutunisha Mfuko wa Chama ukishrikiana na Chama au kwa niaba ya Chama.
(iv ) Maombi.
Ungana nasi katika kukiombea Chama.
( v ) Kujitolea.
Unaweza kukisaidia Chama kwa kutoa muda wako na ujuzi wako wakati wowote kukisaidia Chama katika azma ya Kutafsiri, Kuchapisha, Kueneza na katika kuhamasisha watu kutoa kumfidia msomsji apate Biblia kwa bei nafuu.
- Kwanini Chama cha Biblia cha Tanzania kinatoa Maandiko Matakatifu bure kwa baadhi ya watu au vikundi ?
Chama kinatoa Maandiko Matakatifu bure kwa baadhi ya watu wasio na uwezo wa kifedha kumudu kujinunulia,na vile vile ili kukidhi uhitaji wa Maandiko kwa
Watanzania walio wengi kinalazimika kuyauza kwa bei nafuu wanayoimudu ambayo iko chini ya ilyopangwa kuuzia.
- Wito wa Chama kwa Wakristo
Chama kinatoa wito kwa Wakristo wote mmoja mmoja na Makanisa yote kujiunga na kuwa mwanachama wa Chama cha Biblia na kuchangia Chama
fedha ,mawazo nguvukazi na maombi ili kukiwezesha kuendesha kazi zake za Kutafsiri,Kuchapisha na Kueneza Maandiko Matakatifu kwa watu wote
Tanzania.
by The Bible Society of Tanzania | Dec 3, 2018 | Fundraisers, News
ZIARA KATIKA MAGEREZA YA MSALATO NA KONGWA DODOMA
Moja kati ya wajibu muhimu kwa Chama cha Biblia cha Tanzania ni kuhakikisha kuwa watu wote wanapata fursa ya kupata maandiko matakatifu. Kutokana na jukukumu hilo tarehe 27/11/2018 watumishi wa Idara ya Mahusiano na baadhi ya Wale wa Mawasiliano, walipata nafasi ya kutembelea Gereza la Msalato Dodoma na kugawa Biblia, Sabuni na dawa ya meno kwa Wafungwa wa gereza hilo la Msalato. Mkuu wa Gezea la Msalato Afande Huruma Mwakaji akishirikiana na Msaidizi wake na Maafande wengine walitupokea vizuri sana na kutupa ushirikiano wa hali ya juu.

Meneja Mahusiano wa Chama Cha Biblia Rev. Samweli Mshana akikabidhi Biblia na mahitaji mbalimbali ya wafungwa kwa Mkuu wa Gezea la Msalato Afande Huruma Mwakaji

Picha ya pamoja kati ya Watumishi wa Chama cha Biblia, viongozi wa kanisa la KKKT Dodoma na viongozi wa gereza la Msalato
Jukumu la kugawa Biblia halikuishia Gereza la Msalato tu kwani Tarehe 28/11/2018 Meneja Mahusiano na kikosi kazi chake walipata nafasi ya kutembelea Gereza la Kongwa Dodoma. Katika Gereza hili tulipokelewa vizuri sana na kupewa maelezo ya jinsi Wafungwa wanavyohitaji msaada wa Maandiko na vifaa vingne kwani wanatakiwa kjujitegemea.Chama cha Biblia tulifaulu kugawa Maandiko Matakatifu,sabuni, dawa ya Meno na Taulo za akina Mama.Mkuu wa Gereza Afande Nyonyi alishuru sana Chama cha Biblia cha Tanzania kwa msaada huo kwa Wafungwa.

Meneja Mahusiano wa Chama Cha Biblia Rev. Samweli Mshana akikabidhi Biblia na mahitaji mbalimbali ya wafungwa kwa Mkuu wa Gezea la Kongwa Afande Nyonyi

Picha ya pamoja kati ya Watumishi wa Chama cha Biblia, mkuu wa jimbo wa kanisa la KKKT Kongwa (wa kwanza kulia) na viongozi wa gereza la Kongwa