CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA
KUWEZESHA UPATIKANAJI WA MAANDIKO MATAKATIFU KATIKA LUGHA INAYOELEWEKA VIZURI NA KWA BEI WANAYOIMUDU
1.Chama cha Biblia cha Tanzania ni nini?
Chama cha Biblia cha Tanzania ni Shirika la Kikristo lisilo la Kidhehebu lililoandikishwa mwaka 1965 chini ya Sheria ya Udhamini wa Vyama.
Chama cha Biblia cha Tanzania ni Mshiriki wa Muungano wa Vyama vya Biblia ulimwenguni ( United Bible Societies –UBS ) ambao kazi yake kubwa ni uenezaji wa Neno la Mungu kwa wingi na uhakika kama ifuatavyo:
– Kueneza Neno la Mungu katika Lugha na Mawasiliano yanayokidhi mahitaji ya watu wengi Ulimwenguni.
– Kueneza Neno la Mungu katika Tafsiri sahihi bila kupoteza uhalisi wa Maandiko Matakatifu.
– Kuyauza Maandiko kwa bei wanayoimudi ili waweze kulifahamu Neno la Mungu.
- Kaziya Chama cha Biblia ilianza lini Tanzania?
( i ) Wamisionari wa kwanza kabisa nchini Tanganyika ndio walioanzisha kazi ya Chama kwenye karne ya 19.
( ii ) Kazi ya kueneza Biblia iliendelea kukua na mwaka 1982 Chama kilifikia ngazi ya kuwa Mshiriki wa Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni na mwaka 1988 Chama kilipata uanachama kamili wa Muunganohuu.
3.Je kazi za Chama cha Biblia cha Tanzania ni zipi?
Chama cha Biblia cha Tanzania ni chombo cha Kanisa kinachotumika katika kutekeleza utume wa Kanisa wa kuihubiri Injili kwa kila mtu. Chama cha Biblia kinafanya yafuatayo:
a ) Kutafsiri Biblia katika Lugha mbalimbali za kienyeji.
b ) Kuchapisha katika Mitindo mbalimbali:
– Biblia nzima.
– Maagano na
– Sehemu zake kwa wasomaji wapya.
c )Kueneza Biblia,Maagano na sehemu zake kwa watu wote kwa kushirikiana na :
– Makanisa na Mashirika yake.
– Maduka ya Vitabu.
– Watu binafsi pamoja na wakereketwa wa kujitolea.
d )Kushirikiana na Vyama vingine katika kuhakikisha Biblia inasomwa kwa lugha zote za hapa Tanzania ili kila mtu auonje uzuri wa Yesu Kristo na kupata maisha mapya.
- Je, hadi sasa Chama cha Biblia cha Tanzania kimetafsiri Biblia katika Lugha zipi za kienyeji ?
Chama hadi sasa kimemudu kutafsiri Biblia nzima katika Lugha za: Kiiraqw, Kihaya, Kinyakyusa, Kisukuma, Kijaluo, Kimasai na Kigogo. Pia kimeweza kutafsiri Agano Jipya katika Lugha za Kibena, Kimashami, Kivunjo, Kimochi, Kichasu( Kipare ), Kijita, Kidatooga, Igikuria, Kishambala, Kizaramo, Kinyiramba na Kirimi ( Kinyaturu ) Miradi ya Tafsiri inayoendelea ni ya Lugha za Kihehe, Kikaguru, Kiha na Kisukuma cha kisasa. Mbali na kuchapisha Biblia, pia Chama kinachapisha matoleo yafuatayo:
– Sehemu za Biblia.
– Sehemu za Biblia kwa wasomaji wapya wanaojifunza Biblia kwa Kiingereza, Kiswahili na Lugha za Kienyeji.
– Vipeperushi maalum vya vifungu vya Biblia kwa matukio mbalimbali k.m kuzaliwa kwa Yesu,kifo cha Yesu,wagonjwa waliolazwa,na matukio mbalimbali k.m Uhuru, Rushwa nk.
– Kanda naswa za Neno la Mungu.
– Neno la Mungu katika Braille kwa wasomaji wasioona.
– Neno la Mungu kwa maandishi makubwa kwa wenye udhaifu wa macho.
Kwa kawaida tafsiri inafanywa kutoka katika Lugha za asili za Kiyunani na Kiebrania,na hivyo kazi ya Tafsiri ni ngumu, inahitaji uangalifu wa hali ya juu na
inachukua miaka kati ya 8 hadi 10 kutoa toleo moja, kama kuna watafsiri walioajiriwa kwenye mradi kwa wakati wote na kuna wachambuzi 10-15.
- Je Chama cha Biblia kinapata wapi fedha za kukiendesha?
Chama cha Biblia cha Tanzania kinaendeshwa kwa michango ya
– Makanisa.
– Taasisi mbalimbali za Makanisa.
– Watu binafsi ambao ni wanachama.
– Marafiki wa Chama.
– Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni ambao unatoa misaada ya Maandiko Matakatifu kutoka nje ambayo Chama kinayauza na kutumia sehemu ya mapato kuendesha huduma.
- Je Chama cha Biblia cha Tanzania kina mahitaji gani?
Ili kutekeleza kazi zake za Kutafsiri, Kuchapisha na Kueneza Maandiko Matakatifu Chama cha Biblia chaTanzania kinahitaji kiasi kisichopungua Dola Milioni moja za Marekani kwa mwaka. Kama Kanisa na Wakristo binafsi watakuwa wanachangia kila mwaka kwa uaminifu Chama kinaweza kuendesha kazi zake vizuri.
- Je, unawezaje kusaidia kazi za Chama cha Biblia ?
Kuna njia nyingi za kukisaidia Chama cha Biblia katika kazi zake na kinamualika kila Mkristo kushiriki yafuatayo:-
( i )Kujiunga na kuwa Mwanachama na kuchangia
– Uanachama wa Maisha Mme na Mke shilingi 15,000= na ahadi isiyopungua shilingi 15,000=kwa mwaka.
– Uanachama wa Maisha mtu mmoja shilingi 10,000= na ahadi isiyopungua shilingi 10,000= kwa mwaka.
– Uanachama wa kawaida (bidii ) shilingi 5,000=kwa mwaka.
– Uanachama wa kawaida kwa Wanafunzi wa Sekondari na Vyuo shilingi 2,000= au zaidi kwa mwaka.
– Uanachama wa kawaida wa kushirikishwa kwa watoto na wanafunzi wa shule za Msingi shilingi 1,000= au zaidi kwa mwaka.
– Uanachama wa Mashirika shilingi 50,000= na mchango usiopungua shilingi 50,000= kwa mwaka.
– Mwanachama wa Biblia Moja kwa Mwezi ( Bible a Month Club) 5,000=, 10,000=, 15,000=, 20,000= au zaidi kwa mwezi.
(ii )Tafsiri.
Unaweza kusaidia Chama kwa :
– Kuchangia Miradi ya Tafsiri kwa kutoa fedha taslimu.
– Kuchangia Miradi ya Tafsiri kwa kuwapata Watafsiri wenye uwezo na Wachambuzi wenye mzigo na kazi hii.
– Kuchangia Miradi ya Tafsiri kwa kupitia Miswada ya Tafsiri.
(iii ) Uhamasishaji.
-Kutoa sadaka au michango kila mara kwa Chama.
– Kuhamasisha Makanisani juu ya Wiki ya Biblia ambayo ni kila wiki ya kwanza ya Mwezi Novemba kila mwaka.
– Kuanzisha Vikundi vya Biblia Moja kwa Mwezi ( Bible a Month Club-BAMC ) kwenye Makanisa na maeneo ya kazi.
– Kusaidia kueneza Biblia kwa njia ya kuuza kwa kujitolea.
– Kutoa njia mbadala au mawazo ya jinsi ya kutunisha Mfuko wa Chama ukishrikiana na Chama au kwa niaba ya Chama.
(iv ) Maombi.
Ungana nasi katika kukiombea Chama.
( v ) Kujitolea.
Unaweza kukisaidia Chama kwa kutoa muda wako na ujuzi wako wakati wowote kukisaidia Chama katika azma ya Kutafsiri, Kuchapisha, Kueneza na katika kuhamasisha watu kutoa kumfidia msomsji apate Biblia kwa bei nafuu.
- Kwanini Chama cha Biblia cha Tanzania kinatoa Maandiko Matakatifu bure kwa baadhi ya watu au vikundi ?
Chama kinatoa Maandiko Matakatifu bure kwa baadhi ya watu wasio na uwezo wa kifedha kumudu kujinunulia,na vile vile ili kukidhi uhitaji wa Maandiko kwa
Watanzania walio wengi kinalazimika kuyauza kwa bei nafuu wanayoimudu ambayo iko chini ya ilyopangwa kuuzia.
- Wito wa Chama kwa Wakristo
Chama kinatoa wito kwa Wakristo wote mmoja mmoja na Makanisa yote kujiunga na kuwa mwanachama wa Chama cha Biblia na kuchangia Chama
fedha ,mawazo nguvukazi na maombi ili kukiwezesha kuendesha kazi zake za Kutafsiri,Kuchapisha na Kueneza Maandiko Matakatifu kwa watu wote
Tanzania.