UZINDUZI WA KITABU CHA KWANZA NA CHA PILI CHA SAMWELI KWA LUGHA YA CHASU
Kanisa la KKKT Usharika wa Hedalu, Dayosisi ya Pare – 20 Oktoba 2024

Wapendwa waalikwa walikusanyika leo kwa tukio la kihistoria la uzinduzi wa kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Samweli vilivyotafsiriwa kwa Lugha ya Chasu (Kipare). Uzinduzi huo uliandaliwa na Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kushirikiana na makanisa ya Kikristo yaliyoko katika wilaya za Mwanga na Same Mkoa wa Kilimanjaro, na kuongozwa na Mratibu wa Mradi, Mchungaji Elineema Mndeme.
Mchungaji Mndeme aliwashukuru wageni wote walioshiriki kwenye tukio la uzinduzi, wakiwemo Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, Mchungaji Timothy Msangi, na Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Pare, Mchungaji Ibrahim Ndekia. Pia aliwapongeza wawakilishi kutoka Chama cha Biblia cha Tanzania, akiwemo Katibu Mkuu, Dkt. Alfred Kimonge, kwa kuwezesha kazi kubwa ya kutafsiri Biblia kwa lugha ya Chasu.


Kazi ya tafsiri imefanywa kwa ushirikiano wa wataalamu wa lugha, viongozi wa makanisa, na wahakiki wa tafsiri. Mchango mkubwa ulitolewa na Meneja wa Tafsiri, Dada Leah Kiloba, na washirika wake katika Chama cha Biblia cha Tanzania, pamoja na wataalamu wa teknolojia ya taarifa Felix na Charles, ambao waliweka mifumo ya tafsiri katika kompyuta.
Kwa upande wa usimamizi wa tafsiri, Dkt. Chris Pekka Wilde, mshauri wa mradi, ametajwa kwa mchango wake wa kiufundi na ushauri thabiti katika kuhakikisha tafsiri zinafuata viwango vya juu.
Mradi wa kutafsiri Biblia kwa lugha ya Chasu unahusisha watafsiri wanne: Mchungaji Elineema Mndeme (Mratibu), Mchungaji Joasi Mpinda, Mchungaji Msifuni Msuya, na Mchungaji Imani Chediel Mgonja. Wahakiki wa tafsiri wamejumuisha wachungaji na wainjilisti na wajumbe raia kutoka maeneo mbalimbali ya jamii ya Chasu.



Mpaka sasa, nusu ya vitabu vya Agano la Kale vimetafsiriwa. Kazi ya tafsiri inapitia hatua nne: kwanza, mtafsiri anatafsiri kitabu chake; pili, watafsiri wote wanakipitia; tatu, wahakiki wa jamii wanakikagua; na mwisho, mshauri wa kitaalamu anakihakiki.
Vitabu vilivyokamilika mpaka ngazi ya mshauri ni Ruthi, Yona, Yoshua, Waamuzi, Kitabu cha Nyakati 1 na Nyakati 2, Kitabu cha Wafalme 1 na Wafalme 2, Esta, Mwanzo, pamoja na Kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Samweli ambavyo vimezinduliwa leo rasmi.


Aidha, Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kiko kwenye ngazi ya uhakiki, na kinatarajiwa kufika kwa mshauri mwezi Novemba. Kitabu cha Hesabu kiko katika hatua ya kuratibu, huku vitabu vya Kutoka, Mambo ya Walawi, Nehemia, na Ezra vikiwa katika hatua ya awali ya tafsiri.
Mchungaji Samweli Mshana kutoka Chama cha Biblia cha Tanzania alitoa hotuba fupi akieleza majukumu makuu ya Chama hicho, ambayo ni kutafsiri, kuchapisha, kusambaza Biblia, na kutafuta rasilimali fedha ili kupunguza gharama za shughuli hizo kwa njia ya uchangishaji fedha (fundraising).
Aliwasihi Wakristo kujiunga na Chama cha Biblia cha Tanzania ili kusaidia kupunguza bei za maandiko, hususani kwa ajili ya wafungwa na jamii zinazoishi katika hali ngumu.



Pia katika Ibada hiyo alikabidhi redio 60 zenye Biblia kwa lugha ya Chasu, zinazojulikana kama mpiga mbiu (proclaimer), na kuomba viongozi wa Kanisa waziweke wakfu kwa matumizi ya kanisa. Pia aliwahimiza kusimamia mradi wa “Imani Huja kwa Kusikia” kwa kuanzisha vikundi vya kusikiliza, na akawakumbusha kutuma ripoti za maendeleo ya vikundi hivyo.
Mchungaji Mshana pia aliwaomba viongozi wa makanisa kuzindua kitabu cha kwanza na cha pili cha Samweli vilivyotafsiriwa kwa lugha ya Chasu kama ishara ya hatua kubwa iliyofikiwa katika mradi huo.

Tukio hili limekuwa la mafanikio makubwa na linaashiria mwanzo mzuri wa upatikanaji wa Biblia kwa Lugha ya Chasu, jambo ambalo litasaidia sana kueneza Neno la Mungu kwa ufasaha katika jamii hiyo.
Join
Work With Me

0 Comments