UZINDUZI WA BIBLIA YA KIKAGULU – WILAYA YA GAIRO, MKOA WA MOROGORO.
Tarehe: 8 Juni 2025
Mahali:Gairo, Morogoro
Uzinduzi wa Biblia ya Kikagulu Unasisitiza Uthamini wa Lugha za Asili

Dr. Alfred Elias Kimonge akikabidhi Biblia kwa ajili ya kuzinduliwa.
Ibada na kubariki wa Biblia.
Ibada ya uzinduzi na kubariki Biblia iliongozwa na Askofu Godfrey Sehaba wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro. Pia, viongozi wengine wa kidini waliohudhuria ni pamoja na Mch. Stanley Makasi Tabulu (Msaidizi wa Askofu KKKT), Askofu Frederick Chingwaba (Kanisa Huria Anglikana Tanzania) na Msaidizi wa Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro.
Chama cha Biblia cha Tanzania (BST) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kiimani na kijamii, tarehe 8 Juni 2025, ilifanikiwa kufanya uzinduzi wa Biblia kwa lugha ya Kikagulu, katika Wilaya ya Gairo, Mkoa wa Morogoro.
Hafla hii ya kihistoria iliongozwa na Mheshimiwa Lay Canon Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza lugha za asili za Kitanzania.

Askofu Godfrey Sehaba akifanya uzinduzi wa Biblia ya Kikagulu


Mhe. Prof. Kabudi akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi Biblia mpya ya Kikagulu.
Maneno ya Mgeni rasmi
Mheshimiwa Kabudi alibainisha kuwa lugha za asili ni hazina ya taifa na kwamba uandishi na utafsiri wa maandiko matakatifu kwa lugha za asili ni jambo la msingi kwa uenezi wa injili na utunzaji wa utamaduni wa Taifa.
Katibu Mkuu wa Wilaya ya Gairo
Daudi Abdallah Sehaba (DAS wa Gairo) alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mheshimiwa Jabiri Omari Makame, akisifu juhudi za watafsiri, wahariri, na wadau wa kiimani kwa kazi hii kubwa.

Daudi Abdallah Sehaba (DAS wa Gairo)

Mojawapo ya kikundi cha ngoma za asili kikitoa burudani kwenye uzinduzi
Burudani na Furaha ya Wananchi .
Sherehe hiyo ilionyesha utamaduni wa Kikagulu kupitia ngoma na kwaya mbalimbali zilizofurahisha wageni na wananchi wa Gairo. Uzinduzi huo ulikuwa ni sherehe ya kipekee, ikiashiria mafanikio ya miaka ya juhudi za utafsiri na uchapishaji wa Biblia hii.


Shukrani na Tuzo
Mwishoni, Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia Tanzania, Dk. Alfred Elias Kimonge, alitoa shukrani kwa watafsiri na wadau wote waliofanikisha mradi huu wakiwemo Askofu Frederick Chingwaba– Mtafsiri, Askofu Michael Peter Nhonya – Mratibu na Mtafsiri wa Mradi wa Kikagulu na Wahariri wa Biblia ya Kikagulu pamoa na kuwapatia zawadi.



0 Comments