KILELE CHA MAADHIMISHO YA JUMA LA BIBLIA MKOANI DODOMA
Dodoma, 03 Novemba 2024 – Maadhimisho ya kilele cha Juma la Biblia mwaka huu yamefanyika kwa mafanikio makubwa mkoani Dodoma, katika Uwanja wa Mashujaa. Maadhimisho hayo yaliyoanza na maandamano ya amani kutoka makao makuu ya Chama cha Biblia cha Tanzania (CBT) hadi viwanja vya zamani vya Mashujaa, yalivutia umati wa wanachama na wadau mbalimbali. Maandamano hayo yalipambwa na bendi ya tarumbeta na kwaya ya wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), huku wanachama wakivalia tisheti zilizo na nembo ya CBT na kauli mbiu ya mwaka huu: “Neno la Mungu, Maadili Yetu.”
Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Askofu Amos Muhagachi, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CBT, akiwa ameambatana na viongozi wengine wakuu wa Chama akiwemo Katibu Mkuu wa CBT, Dkt. Alfred Elias Kimonge, na Mkurugenzi wa CBT, Dkt. Anna Solo. Pia, sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi wa makanisa, wanachama wa CBT, na wanafunzi wa UDOM.
Katika hotuba yake mgeni rasmi Askofu Amos Muhagachi alisoma Neno la Mungu kutoka Zaburi 119:105, “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu,” akisisitiza umuhimu wa Neno la Mungu kama msingi wa maadili. Alisema, “Biblia ni kitabu kinachotuunganisha sisi Wakristo na kinatuonyesha maisha ya mwanadamu, ukombozi, na umilele wake.” Pia alihimiza mpango mkubwa wa maadhimisho mwaka ujao, kwa kushirikiana zaidi ili kufikia wadau wengi.
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu Dkt. Kimonge aliwashukuru wanachama na wadau wote waliojitolea kushiriki Juma la Biblia lililoanza tarehe 28 Oktoba na kumalizika leo 03 Novemba. Dkt. Kimonge alieleza kwamba lengo kuu la CBT ni kutafsiri, kuchapisha, na kusambaza Biblia kwa watu wote, wakiwemo Wakristo na wasio Wakristo. Alihimiza umoja katika kuchangia kazi hii muhimu, hasa kwa makundi yasiyo na uwezo wa kununua Biblia, kama vile wafungwa na vijana.
Katika kuelezea historia ya CBT, Dkt. Kimonge alitaja hadithi ya binti Maria Jones, mwenye umri wa miaka kumi na tano, aliyekuwa mkulima wa Wales. Kiu yake ya kumiliki Biblia ilichochea harakati za kuanzisha vyama vya Biblia, ambavyo leo vinafanya kazi katika nchi zaidi ya 160, kusambaza mamilioni ya Biblia na maandiko mengine katika lugha zaidi ya 15,000.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa maneno ya shukrani kutoka kwa Meneja wa Mahusiano na Makanisa, Mch. Samweli Mshana, aliyewapongeza viongozi wote kwa kufanikisha Juma la Biblia kwa ufanisi. “Shukrani kwa viongozi wetu na wanachama wote wa CBT kwa kazi kubwa mliyofanya. Mungu awabariki sana,” alisema Mch. Mshana.
Maadhimisho ya Juma la Biblia yanaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya waumini, wadau, na jamii kwa ujumla kupitia Neno la Mungu, na CBT inaahidi kuendelea na jitihada hizi kwa ustawi wa kiroho wa Watanzania.
0 Comments