CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA CHASAMBAZA ZAIDI YA MAANDIKO 538,000 MWAKA 2025
Dodoma, Juni 2026 – Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Biblia cha Tanzania (CBT), Askofu Dkt. Mark Malwa Malekana, amesema Chama hicho kimefanikiwa kusambaza jumla ya maandiko matakatifu 538,544 katika mwaka 2025, ikilinganishwa na maandiko 512,650 yaliyosambazwa mwaka 2024.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa 40 wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Askofu Malekana alisema ongezeko hilo linaonyesha mafanikio ya juhudi za Chama katika kuhakikisha Neno la Mungu linawafikia Watanzania wengi zaidi kupitia mifumo na lugha mbalimbali.
Mbali na ongezeko la usambazaji wa maandiko, Chama hicho pia kimepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi yake mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Bible Plaza, maandalizi ya Kamusi ya Biblia, Itifaki ya Biblia pamoja na uchapishaji wa kitabu cha historia ya Chama cha Biblia cha Tanzania.
Aidha, Chama kimeendelea kuimarisha huduma za tafsiri za Biblia kwa kuzindua Biblia za lugha za Kikagulu na Kihehe, hatua inayolenga kuwafikia waumini wanaotumia lugha hizo za asili na kuongeza ushiriki wao katika kusoma na kuelewa Maandiko Matakatifu.
Askofu Dkt. Mark Malwa Malekana – Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Biblia cha Tanzania (CBT).
Dkt. Kimonge aliongeza kuwa mwaka 2025 Chama kimeendelea kutekeleza mradi wa kuwawezesha wanawake na wasichana zaidi ya 3,200 pamoja na wanaume wanaonufaika na mpango huo katika wilaya za Gairo na Kilosa. Mradi huo unalenga kutoa elimu na kuwawezesha wananchi waliokosa fursa ya masomo kutokana na changamoto za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Dkt. Alfred Elias Kimonge, amesema Chama kimeendelea kuwahudumia watu wenye ulemavu wa macho kupitia utoaji wa Biblia za Nukta Nundu (Braille) pamoja na kuendesha mafunzo ya Trauma Healing kwa jamii zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
Viongozi wa Chama hicho wamewataka wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kueneza Maandiko Matakatifu na kusaidia makundi maalumu yenye uhitaji wa huduma za kiroho na kijamii. Wamesema ushirikiano huo utawezesha kufikiwa kwa jamii nyingi zaidi, hususan maeneo ya vijijini.
Katika Mkutano Mkuu huo wa 40, wajumbe walijadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na mikakati ya maendeleo ya Chama kwa miaka ijayo. Wajumbe mbalimbali walipongeza juhudi za uongozi wa Chama cha Biblia cha Tanzania katika kuhakikisha huduma za Biblia zinawafikia Watanzania wa rika na makundi mbalimbali nchini.
Mkutano Mkuu huo pia ulihudhuriwa na wageni kutoka Chama cha Biblia cha Korea Kusini wakiongozwa na Katibu Mkuu wao. Ujumbe huo ulieleza namna Chama cha Biblia cha Korea Kusini kinavyoendelea kushirikiana kwa karibu na Chama cha Biblia cha Tanzania katika utekelezaji wa huduma mbalimbali za kueneza Neno la Mungu, wakisisitiza kuwa ushirikiano huo umejengwa katika msingi wa urafiki wa muda mrefu na maono ya pamoja ya kuhudumia jamii kupitia Maandiko Matakatifu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Chama cha Biblia cha Tanzania akimkaribisha rasmi Askofu Dkt. Stanley Elilekia Hotay kujiunga na Bodi ya Wakurugenzi baada ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa 40 wa Chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.
Aidha, mkutano huo uliwapa wajumbe fursa ya kuwaaga baadhi ya wakurugenzi wa Bodi waliomaliza muda wao wa uongozi baada ya kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Chama. Waliotunukiwa heshima hiyo ni Mch. Dkt. Anna W. Sollo, Mch. Prof. Godson S. Maanga na Mhandisi Ekael Manase.
Sambamba na zoezi hilo, wajumbe walifanya uchaguzi wa wakurugenzi wapya wa Bodi kuziba nafasi zilizoachwa wazi, hatua inayolenga kuendelea kuimarisha uongozi na utekelezaji wa majukumu ya Chama katika kueneza Maandiko Matakatifu na kuhudumia jamii.
Wakurugenzi wa Bodi waliomaliza muda wao wa utumishi.
Mch. Dkt. Anna W. Sollo
Mch. Prof. Godson S. Maanga
Mhandisi Ekael Manase


