Nawasalimu wote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, na kipekee ninamsalimu Baba Askofu Nicholaus Nsanganzelu na wote waliongozana naye. Bwana Yesu apewe sifa.

Ninazungumza kwa ridhaa ya Baraza la Wakurugenzi wa Chama cha Biblia cha Tanzania ambao wanawakilisha Kanisa zima hapa nchini yaani madhehebu yote. Mwenyekiti wa Baraza hili kwa awamu hii ni Mhashamu Askofu Mark Walwa Malekana wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).

Chama cha Biblia cha Tanzania ni mwanachama kamili katika Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni (United Bible Societies-UBS). Kusudi la Muungano huu Ulimwenguni kote ni kutafsiri, kuchapisha, kueneza Neno la Mungu (Biblia) kwa lugha anayoweza kuilewa vizuri msomaji na kwa bei anayoiweza. Chama kinajitegemea lakini kinaheshimu mapatano na malengo ya Muungano huo. Vile vile kinazingatia malengo ya Kanisa katika Umisionari na Uinjilishaji. Makusudi ni kwamba Kanisa lijihusishe katika kukibeba, kukiombea, kuchangia gharama kwa njia ya sadaka maalumu na vile vile kuhimiza uenezaji na usomaji wa Maandiko Matakatifu.

Malengo hayo yanatokana na utume wa Bwana Yesu asemapo, “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math: 28: 19). Hivyo Chama kinafanya juhudi ya kuwapatia watu wote Neno la Mungu katika lugha zao bila nyongeza au kipunguzi katika maana, na kwa bei ambayo walengwa wataimudu.

Ili kutimiza lengo hili Chama cha Biblia, kinatafsiri Biblia au sehemu zake kutoka lugha za awali (Kieberania na Kiyunani) kwenda katika lugha lengwa na kisha kuchapisha na kueneza Neno kwa walengwa. Malengo haya yanafanyika kwa kushirikiana na Kanisa na vyombo vyake. Mara nyingi Kanisa ndilo linaona umuhimu wa kutafsiri na kukiomba Chama cha Biblia kifanye kazi hiyo ya kutafsiri. Kwa hiyo Chama cha Biblia ni mtumishi wa Kanisa. Ni nani anayestahili kupatiwa Neno la Mungu? Ingewezekana, kila mtu apatiwe Neno la Mungu katika lugha yake ili apate nafasi ya kuusikia ujumbe wa kwamba Yesu Kristo pekee ndiye njia, kweli na uzima: ndiye Mwokozi.

Binadamu wamegawanyika katika makundi mbalimbali na tofauti. Makundi hayo yanatambuliwa kama makabila yenye lugha maalum, mengine yana utaifa, mengine yanajitaja kwa njia ya koo, n.k. Ijapokuwa makundi hayo yanatambuliwa hivyo, kunakuwepo sababu nzuri kama za uzalendo zinazoyachukulia makundi hayo kwa pamoja kama ni kitu kimoja. Hata hivyo kama vile ukuta imara unavyotokana na matofali moja moja yaliyo imara, hivyo na watu wenye utambulisho wao wa pekee kwa pamoja wanajenga jamii/taifa imara. Watu wanaimarishwa na tofauti zao. “Katika tofauti zetu tunapata uimara” Katika Ufunuo wa Yesu Kristo (Ufu. 7:9-12) tunaona jinsi wakombolewa wote walivyo pamoja katika halaiki ya mwisho, ijapokuwa ziko tofauti dhahiri kati yao.

Umoja wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni unatambua na kuheshimu tofauti zilizopo baina ya makundi ya watu. Hivyo pale watu wanapofikishiwa Neno la Mungu na ikadhihirika kuna udhaifu wa kulisoma, basi hatua zinachukuliwa ili kulihimiza Kanisa liwawekee watu misingi ya kujua kuisoma na kuiandika lugha yao. Matokeo ni kwamba kwa kuijua lugha yake kwa kulisoma Neno la Mungu kunamuwezesha mtu kujifunza lugha nyingine. Hivyo kwa kushirikiana na Kanisa, tafsiri mpya za Biblia zinaambatana na juhudi za kuwafundisha watu wazima kwa wadogo, kuisoma Biblia yao. Juhudi hii imefanyika kwa Wasukuma, Wamaasai, Wanyakyusa, Wairaqw na Wachagga. Mikakati ipo kwa Wakaguru, Wagogo, Wahehe, Wadatooga na penginepo ambapo juhudi ya kutafsiri Biblia inaendelea.

Kwa makundi haya Chama cha Biblia kinachukua juhudi zote kuandaa na kuwafikishia watu Biblia iliyoandaliwa katika mifumo tofauti. Kwa mfano, Neno lililochapishwa –(“Printed Format”), Neno lililowekwa katika kanda-naswa – (Magnetic au digital cassette), Neno lililoingizwa kwa njia simulizi – (Audio-Aural-Visual Scriptures), Neno katika mifumo maalumu kama vile Braille kwa Wasioona, New Reader Scriptures kwa wasomaji wa awali, Neno katika mfumo wa Maandishi Makubwa kwa ajili ya Wazee na wengine wenye udhaifu wa macho, Neno katika Matoleo ya Watoto, Neno kwa njia ya Scripture Literacy Promotion, Neno katika Digital Bible Library.

Huduma hii ni kwa ajili ya Kanisa, ili liweze kutumia zana hizo katika kuyatunza makundi hayo yote ya watu walioko katika maeneo yao ya Umisheni.

Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni kutokana na tamko la pamoja imejiwekea Sera ya kutafsiri Biblia aidha kwa mara ya kwanza au kwa kuhariri upya iliyokuwapo, ili angalau ifikapo 2033 makundi au makabila yote;

  • Yanayofikia au kuzidi idadi ya watu 500,000 wapatiwe Biblia nzima.
  • Yanayofikia idadi ya watu 250,000 wapatiwe Agano Jipya.
  • Yanayofikia idadi ya watu 100,000 wapatiwe Kisehemu cha Biblia (Bible Portions).

Hapa Tanzania tumekamilisha tafsiri 43 kati ya lugha 132 kazi inaendelea.

Ieleweke kwamba tafsiri ikianza tu, lengo ni kuikamilisha Biblia nzima hata kama idadi ya wazungumzaji ni ndogo ili asiwepo mtu atakayesema “nimekosa nafasi katika ufalme wake Yesu Kristo kwa kuwa Neno lake halikupatikana katika lugha yangu”

Makanisa kwa kushirikiana ndiyo yanayoomba kuanzisha na hatimaye kukamilisha tafsiri ili kila mtu awe na Biblia yake katika lugha anayoichagua na kuielewa.

Hizi lugha ambazo ni kitambulisho cha kila mtu na lugha yake, zinakabiliwa na changamoto kadhaa, kwa mfano;

  • Kutotiliwa maanani na kupewa kipaumbele na baadhi ya mamlaka tawala na Makanisa.
  • Lugha ya utawala (kama vile Kiingereza, Kiswahili, n.k) inagandamiza lugha nyingine na kuashiria kuitoa.

Neno la Mungu linadumu milele. Kwa hiyo lugha ambayo inalizungumzia Neno la Mungu inadumishwa. Ni wajibu wa Kanisa kuhakikisha Biblia inayozinduliwa inatumika katika ibada zao.

Hapa Tanzania kuna makundi/makabila ya lugha hai 132. Hadi sasa kuanzia 1846 hadi 2020 Chama cha Biblia, kwa kushirikiana na Kanisa tumetafsiri Neno la Mungu katika makabila yafuatayo;

Sehemu Agano Jipya Biblia
1. Swahili Southern 1846
2. Swahili (SUV) 1952
3. Swahili (CL) 1996
4. Wajita 1920 1930
5. Wakuria 1969 1996
6. Wamasai 1905 1923 1992
7. Wadatooga 2002 2009 2020
8. WaIraqw 1957 1977 2003
9. Kivunjo 1966 1999 2020
10. Machame 1932 1999
11. Kimochi 1892 1999
12. Wanyakyusa 1895 1908 1996
11. Wahaya 1920 1930 2001
13. Wasukuma 1895 1925/2001 1960/2020
14. Wakuria 1969 1996
15. Wameru 1964
16. Chasu/Pare 1910 1922
17. Kihehe 1999
18. Kibena 1914
19. Cigogo 1886 1899 2002
20. Kidatooga 2009 2020
21. Kiluo 1953
22. Kinyamwanga 1982
23. Chiyao 1920
24. Kimambwe 1901
25. Kilungu 1901
26. Kishambala 1908
27. Kinyamwezi 1951
28. Kitaveta 1949
29. Kinyiha 1950
30. Kinyiramba 2010
31. Kirimi 2010
32. Kikerewe 1946
33. Kikinga 1961
34. Kizaramo 1975
35. Kifipa 1988
36. Kikaguru 2010
37. Kibondei 1887
38. Kingoni 1891
39. Kizigua 1906
40. Kimpoto 1913
41. Kizinza 1930
42. Kihangaza 1938
43. Kiha 1960
44. Kiwanji 1985
45. Kizanaki 1948

Kazi bado ni kubwa, Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kushirikiana na Kanisa, kinayo mikakati ya kuwafikishia Neno la Mungu makundi/makabila yaliyobaki. Rai yetu kwa Kanisa tunaomba Biblia hii itumike katika ibada ili kazi hii iliyofanyika kwa miaka mingi na kwa gharama kubwa isiwe ya bure.

Leo tumekamilisha jitihada katika lugha ya Kidatooga kwa kuwakamilishia Biblia: Mungu anena na Wadatooga katika ukamilifu wa Biblia ya Kidatooga. Ni matumaini yetu kwamba Injili ya Wokovu katika Yesu Kristo itawafikia katika lugha yao ya moyoni na kusema sasa nimetambua Mungu anasema nami kwa lugha yangu.

Kwa njia ya tafsiri hii ya Biblia, Wadatooga nao watamsikia Bwana Yesu kwa ukaribu wa moyoni ili wapate fursa ya kushiriki katika halaiki ya mwisho “ Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha (Kidatooga)…” (Ufu. 7: 9-12).

Bwana Yesu atubariki sisi sote.

Dr. Alfred E. Kimonge

KATIBU MKUU.

CHAMA CHA BIBLIA CHA TANZANIA.

04 Oktoba, 2020.

× How can I help you?