Kama ilivyosomwa kwetu katika Ibada hiyo ya Uzinduzi na Askofu Julius Nyange Meneja Mstaafu wa Tafsri katika Chama cha Biblia cha Tanzania.
Waheshimiwa Viongozi, Maaskofu, Mapadre, Wachungaji, Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Watendakazi wa Kanisa na Watumishi wa Mungu, Wamishenari, Viongozi wa Serikali na hasa Wakristo na wasemaji wa lugha ya Kidatooga. Ndugu waalikwa wote, Mabibi na Mabwana nawasalimu katika Jina kuu la Yesu Kristo Mwokozi wetu.
Ni furaha kubwa kushuhudia tukio hili kubwa la kihistoria, la Uzinduzi wa Biblia katika lugha ya Kidatooga. Nifuraha kubwa kwetu sote kushuhudia siku hii ya leo.
Wote tunaikumbuka siku kama hii, wakati wa Uzinduzi na kuwekwa wakfu Agano Jipya la Kidatoga, iliyofanyika Oktoba 12, 2009 katika viwanja vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli karibu na Ziwa Basotu, Mbulu.
Tukio la leo ni kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mradi wa kutafsiri Biblia kwa lugha ya Kidatoga.
Sasa jamii yote ya Kidatoga na wasemaji wa lugha yta Kidatoga wataweza kusoma na kumsikia Mungu akiongea nao kwa lugha yao ya moyoni.
Lugha ya Kidatoga ni tawi la familia ya kusini ya lugha ya Kinilotiki (Southern Nilotic language family). Lahaja saba za Kidatoga ni pamoja na – Bajuta, Gisamjaga, Barabaiga, Isimijega na Rotigenga, Buradiga na Bijanjida.
Barabaiga ndilo kundi kubwa zaidi katika familia hii. Wadatoga wakati mwingine hujulikana kama Wamang’ati hasa kwa mujibu wa Wamasai. Mang’ati maana yake ni “adui” ingawa kwa sasa kwa ujumla halitumiki tena, na linasisitizwa lisitumike kabisa. Tunazungumzia Wadatoga.
Historia ya mradi wa Kidatoga imekuwa ndefu na ngumu sana. Lakini tunamshukuru Mungu kwa sababu ya siku hii maalum iliyosubiriwa kwa muda mrefu, sasa imefika.
Mnamo mwaka 1987 shirika la SIL lilitambua uhitaji wa Biblia kwa jamii ya Kidatoga.
Jambo hili lilipelekea kanisa la KKKT Dayosisi ya Mbulu kuwaalika shirika la SIL kuanzisha mradi wa tafsiri ya Biblia kwa Kidatoga. Shirika la SIL likaandaa timu wa tafsiri ambayo iliongozwa na John na Heidi McCauley. Baada ya kipindi kifupi karibu na mwishoni mwa mwaka 1989 John na Heidi McCauley wakabadilishwa na Ralph na Anette Schubert. Kutokana na mabadiliko haya SIL hawakupata msukumo wa kuendelea na mradi huu.
Baadaye, kanisa la KKKT Dayosisi ya Mbulu likakiomba Chama cha Biblia cha Tanzania kuwasaidia. Chama cha Biblia cha Tanzania hakikusita, kiliupokea mradi huu na kuusimamia.
Kwa msukumo na msimamo mkubwa wa aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo Hayati Mch. Albert Mongi alihakikisha kwamba jitihada hizi zinafanikiwa. Uzinduzi rasmi wa Mradi huu ulifanyika katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom, tarehe 14 Januari, 1990.
Timu ya Watafsiri ilikuwa na watumishi wafuatao – Mch. Elikana Gayewi, Mch. Festo Basso na Mch. Joseph Maho. Badaye, Mch. Gayewi aliicha timu lakini Pamoja na changamoto nyingi za kazi hii ngumu, Mch. Maho na Mch. Basso walistahimili na kung’ang’ana kuifanya. Hali kadhalika kwa jitihada za Dr. Isaac Malleyeck za kufanya kampeni kwa ajili ya mradi huu Pamoja na misaada mbali mbalimbali za aliyekuwa kiongozi wa Hospitali ya Haydom, Hayati Dr. Olson na familia yake ilikuwa muhimu sana kwa maendeleo ya mradi. Kwa msukumo mkubwa wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mbulu, Hayati Askofu Yoram Girgis aliyehimiza na kutamani kuona kwamba Wadatoga wanapata Biblia yao ilikuwa zana kubwa katika kusukuma mbele mafanikio ya mradi.
Tahajia (Arthography) ya lugha hii iliyoandaliwa kwa msaada wa Shirika la SIL iliweka msingi wa kazi liyoendelea. Hata hivyo, kabla ya kufikia mwisho wa kazi hii wafanyakazi wa Shirika la SIL wakajitoa. Ndipo baadaye, ikabadilishwa, ikarekebishwa na kukubaliwa.
Haikanushiki kwamba Tahajia itahitaji kuboreshwa siku zijazo
Kwa kweli, ari ya kutafsiri Agano Jipya ilianza tangu mwaka 1998 na kuendelea. Mnamo 2002 Agano Jipya likawa limekamilika. Kazi ya Agano la Kale ikafuatia mara moja. Injili ya Marko ilichapishwa kama Kitabu nakutolewa tayari kwa kusambazwa katika ibada ya uzinduzi iliyofanyika katika Kanisa la Kilutheri karibu na Ziwa Basotu tarehe 7 Julai, 2002. Nakala zote 2000 zilichapishwa na Chama cha Biblia cha Tanzania zilisambazwa mara moja.
Agano Jipya lilichapishwa mwaka 2009 na hatimaye kuwekwa wakf una kuzinduliwa katika sherehe iliyofanyika katika Kanisa la KKKT karibu na Ziwa Basotu mahali palipo na ofisi za Mradi.
Sherehe ile ya vifijo na furaha iliongozwa na Mkuu wa Kanisa la KKKT Dayosis ya Kati Singida Mhasham Askofu E. Sima kwa niaba ya Askofu Zebedayo wa KKKT Dayosis ya Mbulu.
Chama cha Biblia cha Tanzania kiliwakilishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo Mch. Drk Mkunga Mtingele, Pamoja na watumishi kadhaa wa Chama wakiwemo – Alfred Kimonge, John Mnong’one, Mch. (Askofu) Julius Nyange na wengine. Mtaalamu wa Tafsiri kutoka Ofisi Vyama vya Biblia Ulimwenguni Prof. Aloo Osotsi Mojola pia alikuwepo pamoja na wageni wengine kutoka Chama cha Biblia cha Marekani na Ujumbe wa Kilutheri wa Norway.
Tukio la leo, ni kilele cha jitihada zilizoanza miaka mingi iliyopita. Hakika, leo ni siku ya kipekee isiyo na kifani na ya kihistoria. Hii ndiyo siku ambayo wamisionari walioweka misingi ya Kanisa kati ya Wadatoga bila shaka waliiota na kutama kuiona. Sisi tunaishuhudia leo na kwa kweli ni siku ya ajabu nay a kupendeza machoni petu. Jina la BWANA litukuzwe. Mioyo yetu imeja sifa na shukrani nyinge kwa Mungu wetu aliyetuwezesha kuiona siku hii.
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri hapa Mbulu na makanisa mengine yaliyoshiriki wanapaswa kusifiwa na kushukuriwa kwa kazi na jitihada uhudi zao za kuutangaza mradi hadi kufikia siku hii ya leo.
Watafsiri wa Kidatoga na hasa Mch. Joseph Maho, Mch. Festo Basso, Dr Isaack Malleyeck, familia ya Hayati Dr. Olson na Ujumbe wa Kilutheri wa Norway, Chama cha Biblia cha Tanzania Pamoja na watumishi wake, na hasa aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo Mch. Albert Mongi, Mch. Canon Dr. Mkunga Mtingele, Nd. Alfred Kimonge, Mch. (Askofu) Julius Nyange, Mch. Canon Prof. Aloo Osotsi Mojola, Pamoja na wote waliovujajsho kwa namna moja au nyingine kuona kwamba Biblia katika lugha ya Kidatoga – wanapongezwa sana kwa kazi ya upendo.
Sifa na Utukufu apewe Mungu wetu aliye Juu!
Imeandaliwa na Mch. Canon Prof. Aloo Osotsi Mojola. Mtaalamu wa Tafsiri Mstaafu wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni na ambaye kwa sasa ni Profesa wa Falsafa na Mitaala ya Tafsiri, Chuo Kikuu cha St. Paul, Limuru Kenya.