Kama ilivyosomwa kwetu katika Ibada hiyo ya Uzinduzi na Askofu Julius Nyange Meneja Mstaafu wa Tafsri katika Chama cha Biblia cha Tanzania.

Waheshimiwa Maaskofu, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Biblia Cha Tanzania, Katibu Mkuu wa Chama Cha Biblia cha Tanzania, viongozi wa Makanisa na viongozi wa Serikali, waheshimiwa Mapadri, Makasisi na Wachungaji, akina baba na akina mama, ndugu wote katika Kristo Yesu na wageni wote waalikwa, mabibi na mabwana nawasalimu nyote katika jina tukufu la Yesu Kristo.

Leo ni siku ya shangwe, furaha, nderemo na vigelegele, kwa sababu ya tukio hili kubwa la kihistoria linalofanyika leo tarehe 27 Septemba, 2020. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa hapa Kilimanjaro Biblia ya kwanza katika lahaja au msemo wa Kivunjo-Chagga inazinduliwa na kutolewa rasmi na Kanisa kwa wakristo wote wanaoongea na kuelewa msemo huu.

Wamisionari wa Kilutheri, kikundi cha Leipzig, waliofika kwa mara ya kwanza maeneo haya ya Kilimanjaro Tanzania, miaka ya 1890, wakianzia pale Old Moshi, na baadaye Nkwarungo, Mamba, Shira, Mwika, Masama, Uswaa na Marangu; wakiwemo Emil Muller, Gerhard Althaus, Robert Fassman, Albin Boeme na Theodore Passler, bila shaka tukio la leo lilikuwa ndoto yao. Mmoja wao, mmisionari mwanaisimu na mwana-anthropolojia, Bruno Gutmann, aliyepewa jina “Wasahuye a Wachaka” alilipa kipaumbele suala la kuitafsri Biblia katika lugha ya Kichagga. Juhudi za wamisionari Bruno Gutmann, R Fassman pamoja na wazee wenyeji zilizaa matunda kwa machapisho yafuatayo, mnamo mwaka 1905 kitabu cha Injili ya Yohana kilipochapishwa, mwaka 1908 Barua ya Paulo kwa Warumi, mwaka 1911 Injili ya Mariko, na hatimaye mwaka 1939 Agano Jipya la kwanza katika Kichagga ilichapishwa. Kitabu hiki cha Agano Jipya kilichapishwa na Chama cha Biblia cha Wurttemberg, kule Stuttgart, Ujerumani. Toleo la pili lilichapishwa na Chama Cha Biblia cha Tanzania, Dodoma, mnamo 1999.

Kutafsiri Biblia nzima katika msemo wa Kivunjo kulianzishwa mwaka wa 1991 na Chama cha Biblia cha Tanzania chini ya uongozi wa Marehemu Mchungaji Albert Mongi, pamoja na Mshauri wa Tafsiri, Professor Aloo Osotsi Mojola wa United Bible Societies. Agano Jipya la kwanza katika msemo wa Kivunjo lilichapishwa na kutolewa, pale Marangu mnamo Novemba 6, 1999.

Miradi mitatu ya kutafsiri Biblia ya Kimochi, Biblia ya Kimachame na Biblia hii ya Kivunjo yote ilianzishwa mwaka huo huo wa 1991. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa zote zimekamilika karibu wakati mmoja.

Biblia ya Kivunjo ndio ya kwanza kuchapishwa na kutolewa; zingine zitafuata karibuni. Ningependa kuwashukuru Mchungaji John Mlay na Mchungaji Professor Godson Maanga ambao walijitolea pakubwa kukamilisha Biblia hii ya Kivunjo.

Siku ya leo, Septemba 27, 2020 Biblia Takatifu katika lahaja ya Kivunjo inazinduliwa na kuwekwa wakfu. Jina la Mwenyezi Mungu libarikiwe na kupewa sifa.

Hatuna budi kuwashukuru wale wote ambao wamechangia kwa hali na mali kufanikisha kazi hii takatifu na tukufu, wakiwemo wafuatao:

  1. Marehemu Mchungaji Albert Mongi na viongozi wa Vunjo waliounga mkono juhudi hizi za kutafsiri Biblia katika msemo wa Kivunjo.
  2. Wale wote waliohusika katika kuhakiki na kuchambua tafsiri yote ya Biblia hii.
  3. Mtaalam wa kompyuta na mratibu wa kazi za kutafsiri pale Chama Cha Biblia cha Tanzania – Mchungaji (Askofu) Julius Nyange, pamoja na wafanyakazi wa Chama Cha Biblia, Dodoma ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa sehemu ya kazi hii kubwa.
  4. Wataalam na washauri wa tafsiri ya Biblia waliowashauri watafsiri wa Biblia ya Kivunjo katika kukamilisha kazi yao.
  5. Viongozi wa Makanisa walioombea kazi hii pamoja na kuwatembelea watafsiri na kuwatia moyo.

Mwisho, hatuwezi kuwasahau ninyi nyote – hasa walengwa wa Biblia hii, ambao mmefika hapa siku ya leo kushangilia na kupokea Biblia yenu.

Utukufu na sifa na ukuu kwa Mungu peke yake!

Asanteni sana.

(Imeandaliwa na Professor Aloo Osotsi Mojola, Professor of Philosophy and Translation Studies, Limuru, Kenya, Retired UBS Translation Consultant and former Africa Translation Coordinator, United Bible Societies. Worked with the Kivunjo translation team from 1991 till completion of project.)

× How can I help you?