Baada ya miaka mingi, Wachaga wa Wavunjo, wapata Biblia katika lugha yao ya Kivunjo. Katika Sherehe na Ibaada ya uzinduzi wa Biblia kwa Lugha ya Kivunjo zimefanyika katika Usharika wa Samanga, Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Kanisa la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini, Ibaada hii imefanyika September 27, 2020.
Sherehe hizo ziliudhuliwa na Maaskofu wa Makanisa Mbalimbali, Viongozi wa chama cha Biblia cha Tanzania, (akiwepo: Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Chama cha Biblia cha Tanzania, Baba Askofu Mark W. Malekana wa Kanisa la SDA Tanzania), viongozi wa serikali na vyama vya siasa.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhashamu Baba Askofu Fredrick Onael Shoo ndiye aliyekuwa mgeni rasmi na ndiye aliyeongoza uzinduzi huu. Pia aliambatana na Maaskofu wengine wa Kanisa lake na Mhashamu Baba Askofu Amosi Muhagachi wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Jimbo la Kaskazini wakati wa Ibada hiyo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia cha Tanzania akinazungumza kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Biblia cha Tanzania ambao wanawakilisha Madhehebu na Makanisa yote yaliyopo hapa nchini. Alisema mengi akiusio Chama chake na Kazi mbali za Chama na hasa tafsiri mbali zilizofanyika na zinazofanyika kwa kushirikiana na Makanisa na wadau wengine.
Kwanza alisema Chama cha Biblia cha Tanzania ni mwanachama kamili katika Muungano wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni (United Bible Societies-UBS). Kusudi la Muungano huu Ulimwenguni kote ni kutafsiri, kuchapisha na kueneza Neno la Mungu (Biblia) kwa Lugha ambayo mtu anayoweza kuilewa vizuri. Chama cha Biblia ni cha Makanisa yote na Kinajitegemea, lakini kinaheshimu mapatano na malengo ya Muungano wa vyama vya Biblia ulimwenguni. Vile vile kinazingatia malengo ya Kanisa katika Uinjilishaji.Ni vyema Kanisa lijihusishe katika kukibeba, kukiombea, kuchangia Chama Cha Biblia njia ya sadaka maalumu na vile vile kuhimiza uenezaji na usomaji wa Maandiko Matakatifu (Biblia).
Umoja wa Vyama vya Biblia Ulimwenguni unatambua na kuheshimu tofauti zilizopo baina ya makundi ya watu. Hivyo pale watu wanapofikishiwa Neno la Mungu na ikadhihirika kuna udhaifu wa kulisoma, basi hatua zinachukuliwa ili kulihimiza Kanisa liwawekee watu misingi ya kujua kuisoma na kuiandika lugha yao. Matokeo ni kwamba watu hujua Lugha yao na mwisho huweza kulisoma Neno la Mungu. Hivyo kwa kushirikiana na Kanisa, tafsiri mpya za Biblia zinaambatana na juhudi za kuwafundisha watu wazima kwa wadogo, kuisoma Biblia yao. Juhudi hii imefanyika kwa Wasukuma, Wamaasai, Wanyakyusa, Wairaqw, Wagogo na Wachagga. Mikakati ipo kwa Wakaguru, Wahehe, Wadatooga na penginepo ambapo juhudi ya kutafsiri Biblia inaendelea.
Kwa makundi haya Chama cha Biblia kinachukua juhudi zote kuandaa na kuwafikishia watu Biblia iliyoandaliwa katika mifumo tofauti. Kwa mfano, Neno lililochapishwa –(“Printed Format”), Neno lililowekwa katika kanda-naswa – (Magnetic au digital cassette), Neno lililoingizwa kwa njia simulizi – (Audio-Aural-Visual Scriptures), Neno katika mifumo maalumu kama vile Braille kwa Wasioona, New Reader Scriptures kwa wasomaji wa awali, Neno katika mfumo wa Maandishi Makubwa kwa ajili ya Wazee na wengine wenye udhaifu wa macho, Neno katika matoleo ya watoto, Neno kwa njia ya Scripture Literacy Promotion, Neno katika Digital Bible Library.
Mwisho Katibu Mkuu alisema “Kazi bado ni kubwa, Chama cha Biblia cha Tanzania kwa kushirikiana na Kanisa, kinayo mikakati ya kuwafikishia Neno la Mungu makundi/makabila yaliyobaki. Rai yetu kwa Kanisa tunaomba Biblia hii itumike katika ibada ili kazi hii iliyofanyika kwa miaka mingi na kwa gharama kubwa isiwe ya bure.
Leo tumekamilisha jitihada katika lugha ya Kivunjo kwa kuwakamilishia Biblia: Mungu anena na Wavunjo katika ukamilifu wa Biblia ya Kivunjo. Ni matumaini yetu kwamba Injili ya Wokovu katika Yesu Kristo itawafikia katika lugha yao ya moyoni na kusema sasa nimetambua Mungu anasema nami kwa lugha yangu.
Kwa njia ya tafsiri hii ya Biblia, Wavunjo nao watamsikia Bwana Yesu kwa ukaribu wa moyoni ili wapate fursa ya kushiriki katika halaiki ya mwisho” “ Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha (Kivunjo)…” (Ufu. 7: 9-12).
Ili kufanya uzinduzi wa Biblia ni lazima Translation Consultant (TC) amthibitishie Katibu Mkuu kuwa kazi aliyokabidhiwa ni bora na inafaa kwa kuzinduliwa kwa ajili ya kuwapelekea watu na Kanisa. Akisoma risala kwa niaba ya Professor Aloo Osotsi Mojola, Askofu Julius Nyange alielezea changamoto na mafanikio waliyokutana tangu walipoanza tafsiri hadi Biblia hii ya kivunjo inapozinduliwa.
“Kutafsiri Biblia nzima katika msemo wa Kivunjo kulianzishwa mwaka wa 1991 na Chama cha Biblia cha Tanzania chini ya uongozi wa Marehemu Mchungaji Albert Mongi, pamoja na mimi nilikuwa mshauri wa Tafsiri, kutoka United Bible Societies. Agano Jipya la kwanza katika msemo wa Kivunjo lilichapishwa na kutolewa, pale Marangu mnamo Novemba 6, 1999. Na Siku ya leo, Septemba 27, 2020, Biblia Takatifu katika lahaja ya Kivunjo inazinduliwa na kuwekwa wakfu. Jina la Bwana libarikiwe na kupewa sifa”.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Baba Askofu Mark W. Malekana, alipokuwa akizungumza na Kanisa la Mungu, yeye alifafanua umuhimu wa kulisoma Neno la Mungu (Biblia) na kuweka mipango endelevu ya kulisisha kwa vizazi, vijavyo.
Na mwisho alitoa shukurani kwa Mungu na Kanisa kwa kukiwezesha Chama cha Biblia cha Tanzania, Alisema kuwa Kanisa limejitoa sadaka ili kazi ya chama cha Biblia kiweze kufanikisha kazi hii kubwa kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Kisha Baba Askofu Fredrick Onael Shoo Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini baada ya kukabithiwa Biblia hiyo na Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia Alichukua jukumu lake la Kuiweka WAKFU Biblia hii na alisema:
Baada ya kukabidhiwa Biblia hiyo na kuipokea kwa niaba ya Kanisa la Wavunjo, Baba Askofu aliiweka wakfu kwa maneno yafuatayo:-
“Ninaiweka wakfu tafsiri hii ya Biblia kwa lugha ya Kivunjo katika Jina la Mungu Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. AMEN.”
Ni dhahiri kwamba tunachokiweka wakfu leo ni kitabu na makaratasi yake. Kile kilichoandikwa humo tayari ni wakfu. Maandiko yanazidi kusema katika Injili ya Yohana 6: 63, “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima”.
Biblia ina uzima: ina utakaso. Ameni.
Baada ya uzinduzi kufanyika. Waenezaji walianza kufanya kazi yao ya uzinduzi na kazi hii ilienda vizuri sana. Karibu Biblia 1,000 zilinunuliwa siku ile. Unaweza kuangalia katika picha Mbalimbali hapo chini.
Meneja wa Tafsiri wa Chama cha Biblia cha Tanzania, Rev. Ipyana Mwangota, aliwahoji baadhi ya watu mbalimbali waliokuwa wakinunua na kusoma Biblia; Watu hawa walikuwa wenye furaha na wakimshukuru Mungu sana kwa kupata Biblia yao kwa Lugha ya Kivunjo.
Tunapenda kukushukuru na kukutakia Baraka za Bwana, unapoendelea kukiombea na kukichangia Chama cha Biblia cha Tanzania ili kiweze kufikisha Neno la Mungu kwa Watu na makundi mbalimbali hapa Tanzania.
Ameni.